MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUMRUDIA MPENZI WA ZAMANI!

No Comments
Nisiku nyingine tena tunakutana katika safu hii nikiamini umzima na unaendelea vizuri na majukumu yako ya kila siku kama kawaida
.Mimi namshukuru Mungu kwa kila jambo, amenijaalia afya njema na nguvu za kutosha kiasi cha kuweza kukuandikia wewe kile ambacho naamini kina umuhimu katika maisha yako ya kimapenzi.

Leo ningependa tuzungumzie mambo ya kuzingatia kabla ya kumrudia mpenzi ambaye aidha mmeachana, yupo mbali na wewe au umepoteana naye kwa muda mrefu.
Kugombana ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Yawezekana ulikuwa na mwenzi wako ambaye ulimpenda kwa moyo wako wote na sasa mmeachana lakini moyo wako bado unahitaji kuwa naye.
Kutengana kuna mambo mengi, wakati mwingine huenda ilikuwa ni hasira tu. Siku zote baada ya hasira kuisha, moyo hubaki peke yake katika nafasi yake halisi ya kufanya maamuzi.
Hapo ndipo penye lengo la mada yetu ya leo. Kwamba, kwa msingi huo umegundua kumbe mpenzi wako uliyeachana naye, bado unampenda.
Kwamba hata makosa aliyokuwa akiyafanya, ulimsababishia au si makubwa kiasi cha kuachana na badala yake mnaweza kukaaa na kuzungumza kiutu uzima na kuyamaliza.
Upo tayari rafiki? Je, uko katika kundi hilo? Unataka kumrudisha mpenzi wako wa zamani? Kama jibu ni ndiyo basi mada hii inakuhusu.
HAKIKISHA BADO ANAKUPENDA
Kwa utafiti mdogo nilioufanya nimebaini kuwa baadhi ya watu huamini kwamba kurudi kwa mara nyingine kwa mpenzi wa zamani ni kujidhalilisha, kujishusha na kujisalimisha.
Hilo si kweli hata kidogo, kikubwa cha kuzingatia hapa ni moyo. Je, unahisi bado unampenda? Ni kweli naye anakupenda? Kama sifa hizi zipo, hayo mambo madogo ambayo mmetofautiana ni ya kawaida kabisa ambayo mnaweza kurekebishana taratibu.
Kwa msingi huo basi, hakuna tatizo lolote katika kurudiana na mpenzi wako wa zamani, maana tayari mmeshajuana vya kutosha, hivyo kukupa urahisi wa kufanya yale anayoyapenda na kuepuka asiyopenda, jambo litakalozidisha umri wa uhusiano wenu.
HAJAPATA MWINGINE?
Lazima ujue kuhusu historia yake kiuhusiano baada ya kuachana na wewe. Hapo unatakiwa kufanya ushushushu wako kimyakimya bila yeye kujua. Ikiwa ameshatembea na mwingine, maana yake ni mtu asiye na msimamo na huenda anaongozwa zaidi na tamaa za kimwili na si mapenzi ya dhati.
Katika kipengele hiki, ni muhimu sana kujua kama muda huo ambao wewe unahitaji kurudi tena mikononi mwake kama ana uhusiano mwingine. Kimsingi kama atakuwa ndani ya uhusiano, itakubidi uwe mpole.
Unatakiwa kufanya hivyo kwa sababu anaweza kukubali kuwa na wewe wakati akiwa bado hajaachana na mpenzi aliyenaye kwa muda huo, hivyo wewe kuwa kama mwizi tu kwa mwenzako.
Hapo utakuwa katika mapenzi ya kushea, jambo ambalo si zuri kisaikolojia na hata kiafya.
Kumbuka kwamba, unaweza kuwa na mwenzi wako, mkapendana kwa dhati na mkadumu kwa muda mrefu, lakini kwa bahati mbaya mkaachana kwa sababu ambazo mnazifahamu wenyewe.
Katika muda mfupi ambao utakuwa umeachana naye, anaweza kufanya mambo ya ajabu sana. Pamoja na kwamba moyo wako unamhitaji, lakini anaweza kuwa tayari ameshapoteza sifa za kuwa na wewe. Katika hali hiyo, ni sahihi kurudiana naye? Bila shaka jibu hapa ni siyo sahihi.
ANA DHAMIRA YA NDOA?
Huenda uliachana na mpenzi wako lakini bado unaamini ndiye alipangwa kuwa mwenza wako wa maisha, hiyo isiwe sababu, jiulize pia kama na yeye anahitaji kuingia kwenye maisha ya ndoa na wewe.
Nasema hivyo kwa sababu, unaweza kunga’ang’ania kumrudisha mpenzi wako wa zamani kumbe mwenzako anataka kupitisha siku tu na wewe. Hana mpango wa kuishi na wewe kindoa.
Kama utabaini mliachana lakini wote dhamira yenu ni kuoana, basi mrudie lakini kama unahisi ni mtu wa kustarehe tu na wewe na wala si muolewaji/muoaji, sidhani kama itakuwa sawa kumrudia.
HANA KINYONGO?
Wapo ambao wanafikia hatua ya kuachana baada kukoseana tena wakati mwingine makosa makubwa. Kwa maana hiyo kama wewe ndiye uliyemkosea mpenzi wako kabla ya kuanza jitihada za kumrudia, kwanza chunguza kama hana kinyongo na wewe na amekusamehe kutoka moyoni mwake?
Kama bado ana kinyongo na ukalazimisha kurudiana naye, huwezi kulifurahia penzi lenu, itakuwa kila akikumbuka ulivyomkosea anapata maumivu na hawezi kukupenda kwa kiwango kinachotakiwa.
Hayo ni baadhi ya mambo ambayo unatakiwa kuyazingatia kabla ya kurudiana na mpenzi wako wa zamani. Cha kuzingatia sana ni kwamba rudiana na mtu ambaye una imani hamtakorofishana tena na kwamba kuachana kwenu kwa mwanzo kuwe kumewapa fundisho.
Ni hayo tu marafiki, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.
back to top