HAYA NDIYO YANAYOMSHUSHA MWANAMKE KATIKA UHUSIANO MPYA!

No Comments
HABARI zenu wasomaji wa safu hii murua. Leo ni siku nyingine, ambayo tunapeana vitu muhimu kuhusu masuala yetu ya uhusiano wa kimapenzi, iwe urafiki tu au hata wana ndoa!Kuna kitu kimoja, tunakiona kidogo sana,
lakini ni cha msingi sana katika namna ya kuanza kujenga uhusiano mpya wa kimapenzi. Na hapa wanaohusika zaidi ni akina dada.
Mwanaume mmoja alipokea simu kutoka namba asiyoifahamu, alipoitika, mpigaji alikuwa ni mwanamke, lakini baada ya mawasiliano mafupi, ikatambulika kwamba mpigaji alikosea.
“Samahani, itakuwa nimekosea namba,” alisema dada huyo, ambaye sauti yake ilimvutia sana mwanaume aliyeipokea.Baada ya sekunde chache, dada yule akatuma tena ujumbe mfupi wa maneno kusisitiza kukosea kwake namba. Yule jamaa akaanza kujibishana naye kwa ujumbe mfupi hadi baadaye wakajikuta wamekubaliana kuanzisha urafiki wa kimapenzi.
Baada ya hapo wakaendelea kuwasiliana kila siku, wakipigiana simu na kutumiana ujumbe mfupi wa maneno. Baada ya siku tatu, mwanaume akataka waonane ili wakate kiu.
“Hapana kaka, haiwezekani iwe haraka hivi, hata hatujafahamiana vizuri,” lilikuwa ni jibu la msichana kwa mwanaume, ambalo lilimuingia vizuri kiasi cha kumwambia kuwa basi kwa kuwa hawajawahi kuonana, ni vyema basi angalau wakakutana ili kufahamiana.
Wiki moja baadaye, wakielekea katika kupanga siku ya kukutana ili kufahamiana, mwanamke akatuma ujumbe huu.“Samahani dear, naomba niongezee salio nataka kuongea na mama.”
Kaka wa watu, akiwa na hamu ya kumuona mtu mwenye sauti ya kuvutia katika simu, hakusita, akatuma salio la shilingi elfu tano!
Wakapanga siku ya kukutana, mchana wakati wa chakula, wakiahidiana kukutana sehemu moja maarufu sana kwa chakula kizuri jijini Dar, ambako vyakula vya aina mbalimbali hupatikana.
Asubuhi ya siku yenyewe, dada akatuma tena sms iliyosomeka hivi: Sina nauli, nitumie nauli ya kuja.
Kwa kuwa mtafutaji hachoki, jamaa akatuma tena kiasi cha shilingi elfu kumi ili dada aweze kupata usafiri wa kumfikisha eneo la tukio.
Wakakutana. Hakuwa msichana mbaya kwa sura na umbo, ingawa usingeweza kusema ni mzuri pia. Kitu cha kukumbuka hapa ni kuwa mvulana hakuvutiwa naye, lakini kwa kuwa hakutaka kuonyesha hivyo, alizungumza naye vizuri na akaomba kama wangeweza kwenda faragha siku hiyo. Akilini mwake, alifahamu msichana huyo asingekubali!
Kwa muonekano, mwanaume alionekana ni mtu ambaye hela ya kula haimsumbui, dada akavutiwa na hisia hizo. Hakuwa na hiyana, akalikubali ombi lile na baada ya chakula wakachukua teksi na kuelekea walikojua wenyewe kumalizana!
Wadada, ukifuatilia simulizi hii vizuri, hata wewe unaweza kujua kuwa kuna makosa matatu ya msingi, lakini ambayo yanaonekana kuwa ya kawaida, yaliyofanywa na msichana huyu, ambayo yanafanywa na wengi.
Kuomba muda wa maongezi hewani lilikuwa ni kosa la kwanza. Ni sawa, siyo kitu kibaya kumuomba mpenzi wako, lakini katika hali ya kawaida, kumuomba mtu ambaye hata hujawahi kumuona, kunampa unayemuomba maswali mengi ya kujiuliza.
Licha ya vocha, pia nauli. Ni kosa lilelile lakini hili linazidisha mashaka zaidi. Mtu anajenga picha isiyoeleweka, je, msichana anayewasiliana naye ni malaya? Ana dhiki au anampima kuona kama ana hela?
Lakini pia kukubali kwenda faragha siku ya kwanza kuonana. Niseme kuwa vitu hivi vinaonekana kuwa ni vidogo na vinavyofanywa na wasichana wengi, vina athari kubwa sana katika uhusiano.
Mtu anajiuliza, kama hata kabla hawajafahamiana, ameshaanza kuomba nauli na vocha, vipi wakiwa wapenzi, si ndiyo itakuwa zaidi?
Ni vyema kujiepusha na vitu hivi kwa sababu huwezi kujua mtu unayewasiliana naye ni wa aina gani. Wengine hupima kwa vitu vidogovidogo kama hivi, hata kama huna salio, muombe unayemfahamu, siku ya ahadi, mkope hata jirani yako upate nauli kama hauna na usiwe mwepesi wa kukubali tendo katika siku yako ya kwanza kukutana naye!
back to top