FAIDA 6 ZA KUOLEWA NA MUME ALIYEKUZIDI UMRI!

No Comments

Mara nyingi wapo ambao hujikuta njia panda baada ya kudondoka kimapenzi kwa watu ambao wamewazidi umri au kinyume chake.Naamini wengi wamekuwa wakikumbana na mazingira haya na kuhisi itakuwa ni tatizo kwa msichana mwenye miaka 24 kuolewa na mwanaume mwenye miaka 40 na zaidi. Au unaweza kukuta mwanaume mwenye miaka 25 katokea kumpenda mwanamke mwenye miaka 30 lakini anaona kuingia naye kwenye ndoa ni shida.
Kabla sijaenda mbele zaidi naomba nisisitize kwamba, umri si tatizo linapokuja suala la mapenzi. Nilishawahi kusema huko nyuma kwamba, mapenzi hayaangalii umri kama ambavyo hayaangalii pesa.
Kwa maana hiyo unapotokea kumpenda mtu aliyekuzidi umri au mwenye umri mdogo kuliko wewe, swali kubwa la kujiuliza hapo ni je, kweli unampenda kwa dhati? Je, na yeye anakupenda kweli na amekupa nafasi kubwa kwenye moyo wake?
Ukipata jibu la ndiyo lenye uhakika, kubali ndoa wala usihofie maneno ya watu. Wakati unafanya uamuzi huo, kumbuka wapo walioingia kwenye ndoa na vijana wenzao lakini leo hii wanajuta kutokana sarakasi wanazokumbana nazo.
Kutokana na hilo ndiyo maana leo nimeona nikupe faida za kuolewa na mwanaume aliyekuzidi sana umri.
Utadeka sana
Kigezo cha kwamba wewe ni mdogo kwake, atakuchukulia kama mwanaye na itakuwa ni sahihi kabisa yeye kukuita ‘baby’. Utakuwa huru kumdekea na yeye atachukulia kumdekea huko kama sehemu ya mahaba na hapo ndipo penzi litanoga.
Jaribu kufuatilia na utabaini kuwa, waliobahatika kuingia kwenye ndoa na wanaume wenye umri mkubwa wanafurahia maisha sana na wanawashangaa wale wanaong’ang’ania wanaume wenye umri sawa.
Hatakusumbua kwa wivu
Uchunguzi unaonesha kuwa, mwanaume ambaye umri umeenda, si msumbufu wa kumfuatilia sana mke wake. Ule usumbufu wa kila saa kupigiwa simu kuulizwa uko wapi, unafanya nini, na nani ni wa nadra sana.
Kikubwa hapo ni kumfanya tu akuamini kwamba unampenda na huna fikra za kumsaliti kwa wanaume wa rika lako. Pia unatakiwa kutochukulia ile tabia ya kutopenda kukufuatafuata kama chansi ya kumsaliti. Ukimpenda kweli na kumheshimu, atazidi kukupenda na ndoa yenu itadumu.
Atakuongoza kimaisha
Watu wazima wanakuwa na uzoefu mkubwa wa kimaisha. Wamepitia mengi na ni rahisi sana kukuongoza katika misingi sahihi.
Licha ya kuolewa ukiwa na mri mdogo, atakufanya na wewe uanze kujiona mtu mzima na hata mambo ya kitotototo hutakuwa nayo. Atakupa maana ya maisha na yapi myafanye na yapi myaepuke ili muwe na maisha marefu ya furaha na amani.
Atakupenda, hatakusaliti
Fuatilia sana utabaini kuwa, wanaume wenye umri mkubwa wengi hawana mawazo ya kuoa. Wao hasa wale wanaopenda dogodogo watakuwa wakiwabadilisha kila siku kwa kutumia pesa na mali zao.
Yaani hawa hawataki kugandwa. Lakini ukimuona mtu mzima anatangaza ndoa, ujue huyo anakupenda kwa dhati na anataka kutulia na wewe. Maana yake hapo ni kwamba, hataki mara leo yuko na huyu, mara kesho na yule.
Kimsingi watu wazima wengi wanaoingia kwenye ndoa ni vigumu kuwa macho juujuu. Hawatakuwa na kipya wanachokitafuta na ndiyo maana inaelezwa kuwa, wanaoolewa na wanaume waliowazidi umri wengi hawasalitiwi ila wao ndiyo mara nyingi husaliti.
Atakuwa mwalimu wako ‘uwanjani’
Katika hili labda na wewe uwe ni mdogo kiumri lakini katika mambo yetu yalee uwe umezeeka. Kama ni mgeni kabisa kwenye michezo ya kikubwa, yeye atakuwa mwalimu wako mzuri na haitakuchukua muda mrefu kuwa mzoefu.
Mambo ya msingi ya kuzingatia
Kikubwa hapa ni kuhakikisha unampenda kwa dhati na si kumpenda kutokana na mali au pesa zake. Kumbuka mali na pesa ni vitu vinavyoweza kuyeyuka na kujikuta unatoka kwenye ndoa na kuandika historia ya kuachika.
Pia chukulia ni maisha yako. Unaweza kuingia kwenye maisha ya ndoa na mwanaume aliyekuzidi umri watu wakaanza kukusema vibaya. Hilo lisikupe shida, kumbuka hayo ni maisha yako na moyo wako ndiyo ulioridhia kuwa naye.
Mwisho, hakikisha unamjengea imani kwamba umempenda yeye kama alivyo. Mfanye akuamini hata ukiwa mbali na yeye. Hiyo itamfanya akuchukulie wewe tofauti na wasichana wengine ambao wanaingia kwenye ndoa na watu waliowazidi umri lakini wanakuwa si waaminifu.
back to top