MADHARA YA KUWA NA DHARAU

No Comments
Kama nilivyokwisha kuzungumza hapo juu, dharau si tabia nzuri kwa binadamu. Madhara ambayo mtu anaweza kuyapata kama atakuwa na tabia hii ni makubwa  na yanaweza kuathiri maisha yake kwa ujumla ukiachilia mbali uwezo wako wa fedha ulionao, umri wako na elimu uliyonayo.
Binadamu ni watu wa matatizo kila siku, uwe na fedha ama elimu ya aina gani, lakini lazima utapata matatizo ambayo yatahitaji ushirikiano na msaada kwa njia moja ama nyingine.
Unapokuwa na tabia ya dharau ni vigumu sana kupata vitu hivyo kutoka kwa watu wa karibu yako kwani ni wazi kabisa unapokuwa na tabia hii inakutengenezea mazingira ya uadui na chuki dhidi ya watu wengine.
Ifahamike kwamba urafiki pamoja na ukaribu na watu hauwezi kununuliwa. Ni vitu ambavyo vinapatikana kutokana na jinsi unavyojiweka kwa watu. Ukiwa na pesa halafu ukajijengea tabia ya dharau lazima watu watakuchukia kiasi cha kuweza kukufanya ukaichukia dunia.
Wangapi wamekuwa wakijikuta katika matatizo lakini hakuna mtu anayejali wala kuwa tayari kutoa ushirikiano? Niwape mfano mmoja ambao naamini kwamba unaweza kukusaidia sana na kukufanya ukaona madhara ya kuwa na tabia ya dharau.
Mzee mmoja alikwemda kwenye harusi, chakula ambacho kilikuwa kinapatikana ni ndizi na ugali tu kutokana na kipato chao kidogo. Kuonesha jinsi gani mzee yule ana dharau ulipofika muda wa  chakula aliondoka na kudai kwamba hawezi kula chakula kile kwani hakikuwa katika hadhi yake na kuonesha kwamba waliostahili kukila ni maskini wenye njaa.
Watu waliokuwa katika eneo hilo walichukizwa sana na kitendo kile cha kudharau chakula kile na kuwadharau pia waliokuwa wamehudhuria katika sherehe kwa kuwaona kuwa ni maskini sana na wenye njaa. Baada ya siku chache yule mzee aliandaa sherehe ya kumpongeza mwanaye baada ya kumaliza masomo yake ya chuo kikuu.
Watu kama kawaida walikwenda wakashiriki kisha ulipofika wakati wa kula waliondoka na kudai kwamba walikuwa wameshiba na kumuacha mzee yule na chakula chake kingi ambacho alikuwa amekiandaa na kushindwa kujua akifanye nini. Hilo lilikuwa ni fundisho kwa mzee huyo na ilikuwa ndiyo mwisho wa tabia yake ya kuwa na dharau.
Unapokuwa na dharau pia unaweza kukosa marafiki. Hakuna anayependa kuwa na rafiki mwenye tabia ya dharau. Wenye dharau wanakuwa ni kama watu wenye ukoma katika jamii. Kila mtu anaweza kuona kwamba kujenga urafiki na wewe anaweza kuirithi tabia hiyo hivyo kutokuwa tayari kuwa rafiki mwenye tabia hiyo.
Kwa kumalizia niseme kwamba maisha mazuri ni yale yaliyojaa furaha. Huwezi kuwa na furaha kama utakuwa na tabia ambazo haziwafurahishi watu hivyo jaribu kujijengea tabia ambazo zitakufanya kuwa karibu na kila mtu na watu kufurahia kuwepo kwako usije ukajikuta umebahatika kupata kila kitu muhimu katika maisha lakini watu walio karibu yako wanakuona kama ugonjwa wa ukoma.
back to top