KAMA NINGEKUWA STEVE NYERERE NINGE…

No Comments
Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity, Steven Mengere ‘Nyerere’.
KWAKO,
Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity, Steven Mengere ‘Nyerere’. Bila shaka mambo yako yapo safi kabisa. Kuna mambo nataka kukushauri lakini nimeona njia hii ya barua ni nzuri zaidi, maana hutaisoma peke yako.

Aisee naitamani sana nafasi yako, maana  ningefanya mengi sana, lakini kwa kuanzia ningeanza na haya yafuatayo ambayo naamini yangesaidia kupatikana kwa mafanikio chini ya uongozi wangu.
Kwa muda mrefu sana kumekuwa na maneno kuhusu nidhamu kwa wasanii wa filamu, hasa wa Bongo Muvi...hapo ndipo sehemu ya kwanza kabisa ambayo ningeanza kuifanyia kazi. Ningeweka mikakati na sheria ndogondogo za kulinda maadili kwa wasanii wa klabu yangu.
Ningepiga marufuku wanachama kuja kwenye mikutano yetu Leaders Club na nguo zinazoacha sehemu ya miili yao wazi. Sheria hii ingeendelea kuwabana hadi wakiwa mitaani, msanii wangu  akikutwa amevaa hovyo mitaani, atakiona.
Wasanii wangu ni kioo cha jamii bwana, hata wakienda klabu wavae nguo za usiku lakini siyo za kuwashushia heshima. Nikimbaini tu mwanachama wangu aliyevaa nusu utupu, rungu la adhabu linamwangukia.
Hata kwenye filamu, ningesisitiza wasanii wakiwa location wavae nguo zenye staha – labda kidogo kwenye stori ambayo itamuonyesha mhusika labda ni kahaba n.k. Kwa kifupi, ningekuwa mkali sana kwenye suala la maadili kwa ujumla wake.
Ningedili pia na suala la usambazaji, ama ningetafuta wafadhili ambao wangetusaidia kusambaza filamu zetu kwa mikataba yenye uhai au ningeitisha mkutano na wasambazaji wa filamu Bongo na kujadiliana namna ya kuboresha mikataba ya kusambaza kazi za wasanii.
Kama yote hayo yangeshindikana, ningehamamisha tuanze kusambaza filamu zetu wenyewe maana hata mmoja wa viongozi wenzangu ndani ya Bongo Muvi, William Mtitu amejaribu. Ningemwuliza amejifunza nini? Kama kuna dalili za mafanikio, tungeanzia hapo.
Ningehubiri sana kuhusu ushirikiano na mshikamano. Ningesisitiza wasanii tusaidiane na tuwe pamoja kwenye kipindi cha raha na shida. Makundi yasingetakiwa kabisa. Msanii ambaye angeonekana kuwa na dalili za kuanzisha makundi, ningemfukuza uanachama haraka sana.
Mwisho kabisa ambalo pengine ndiyo limebeba yote hayo, ningeshirikiana na Shirikisho la Filamu Tanzania ‘TAFF’ kwa karibu. Ningeheshimu mamlaka ya shirikisho hilo, maana ndiyo mama wa wasanii wote wa filamu nchini.
Kwa sababu TAFF inatambulika kisheria, bila shaka ningeweka ukaribu na mwenyekiti wake Simon Mwakifwamba ili nimshauri namna ya kuyashughulikia haya yote.
Ningehamasisha wanachama wangu tufanye namna ili kundi letu lisajiliwe Basata halafu tuwe wanachama wa TAFF. Naamini kwa kufanya hivyo, ningekuwa nimewasadia wanachama wangu na klabu nzima kwa jumla.
Kama ningekuwa ni mimi, ningeanza na mambo hayo. Lakini kwa sababu mimi siyo mwenyekiti wa Bongo Muvi, namwachia Steve Nyerere aamue mwenyewe.
Steve, muda unakimbia sana, umeanza uongozi Januari mwaka huu, tayari mwezi wa tatu unayoyoma huo. Umeifanyia nini klabu? Kazi kwako.
Yuleyule,
Mkweli daima,
Joseph Shaluwa
back to top