TAMASHA LA USIKU WA MATUMAINI 2014 NI VITA

No Comments
Umewahi kujiuliza nini kitatokea endapo waheshimiwa wabunge, Hamis Kigwangala wa Nzega na Mwigulu Nchemba wa Iramba Magharibi wakiziweka suti zao pembeni na kupanda ulingoni, nani atamkalisha mwenzake? Itakuwa vita!

D.k Hamis Kigwangala mbunge wa Nzega.
Basi hicho ndicho kitakachotokea kwenye Tamasha la Usiku wa Matumaini litakalotimua vumbi Agosti 8, 2014 (Nane Nane) kwenye Uwanja wa Taifa ambapo waheshimiwa hao watanyukana live ulingoni katika pambano lisilo la ubingwa kumsaka mshindi.
Achilia mbali wabunge hao, pia mastaa kibao watakung’utana; Jacqueline Wolper atapanda ulingoni dhidi ya msanii mwenzake wa kike, Cloud 112 wa Bongo Muvi na Jacob Steven ‘JB’ nao
watavurumishiana makonde bila kumsahau mwanamuziki wa Mapacha Watatu, Khalid Chokoraa atakayezichapa na Said Memba huku mashabiki watakaohudhuria pia wakipata burudani ya ndondi kali kutoka kwa Bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Thomas Mashali dhidi ya Mada Maugo.
Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo, shughuli haitaishia hapo kwani kutakuwa na burudani ya muziki wa Injili. Watumishi wa Mungu wanaoimba nyimbo za Injili, Upendo Nkone, Ambwene Mwasongwe, Angela, Paul Clement, Martha Mwaipaja na wengine wengi watakuwepo uwanjani hapo.
Mbunge wa Iramba Magharibi Mwigulu Nchemba.
“Pia mkali wa ngoma ya Johnny, Yemi Alade kutoka nchini Nigeria atakuwepo ndani ya nyumba kuoneshana kazi na Zuwena Mohamed ‘Shilole’, achilia mbali Ali Kiba atakayezikonga nyoyo za mashabiki wake waliommisi kwa kipindi kirefu,” alisema Maloto.
Pia aliongeza kuwa kutakuwa na wasanii wengine kibao wakiwemo Madee, R.O.M.A Mkatoliki, Meninah, Juma Nature na kundi zima la Wanaume Halisi na kwa mara ya kwanza Wema Sepetu atapanda jukwaani na kuimba nyimbo za bebi wake ‘Diamond.’
Kwa upande wa soka, Maloto alisema kutakuwa na mechi kati ya Wabunge Mashabiki wa Yanga dhidi ya wenzao wa Simba, timu ya Bongo Muvi itapepetana na Bongo Fleva sambamba na Azam watakaokipiga dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Maloto aliongeza kwamba mshindi wa Shindano la Amani Talent Search, Paschal Dominic ‘P-Plan’ naye ameongezwa kwenye listi ya wasanii watakaomua kwenye shoo hiyo kubwa na ya kihistoria.
Tamasha hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Vodacom, Pepsi, Azam TV, E FM (93.7), Clouds FM (88.5), Syscorp pamoja na Times FM (100.5).
back to top