MPENZI YUKO MBALI? SHEREHEKEA NAYE SIKUKUU KWA STAILI HII!

No Comments


Leo nataka kuzungumzia namna unavyoweza kusherehekea Sikukuu ya Idd wakati mpenzi wako akiwa mbali na wewe.
Nafanya hivi nikiamini wapo ambao wapenzi wao wako mbali na kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao hawawezi kujumuika nao.
Najua namna ambavyo sikukuu inaweza kuwa mbaya kwa kiasi f’lani kwa kumkosa uliyetokea kumpenda lakini kwa kuwa imetokea hivyo, chukulia ni hali ya kawaida ila kuna mambo kadhaa ambayo unaweza kuyafanya ili uwe na furaha siku hiyo.
MawasilianoHakikisha siku hiyo simu yako ina muda wa maongezi wa kutosha na chaji iko ‘full’. Hii ni kwa sababu mawasiliano ya mara kwa mara lazima yafanyike. Kwa siku hii haiwezi kuwa kero, mpigie simu kila unapojisikia na yeye kwa kuonesha kukujali anatakiwa kupokea.
Pia sms nzuri ndiyo wakati wake. Muandikie nyingi kadiri unavyoweza na yeye pia ili kukufanya ujisikie mwenye amani, atatakiwa kukujibu haraka iwezekanavyo.
Hii ni mbinu ya kujiweka karibu naye na endapo utaitumia simu yako ipasavyo, hutajisikia mpweke na siku yako itapita huku ‘ukiwa na mpenzi wako’.
Zawadi!
Hiki ndiyo kipindi chake. Siku hii muandalie zawadi ambayo itamfanya ajione umemthamini sana. Zipo zawadi zinazoshauriwa kwa kipindi hiki cha sikukuu.
Kwa mfano, unaweza kumnunulia nguo, viatu, vipodozi na vitu vingine ambavyo atavitumia siku hiyo. Kwa zawadi hizo ni lazima popote atakapokuwa atajisikia yuko nawe.
Jua atatoka na nani kwenda wapi
Ni vizuri sana kujua huko aliko atatoka na nani kwenda wapi. Katika mazingira haya siyo mbaya kufanya ushushushu kujua kama atakavyokuambia ni sahihi.
Ni vizuri pia huyo anayetoka naye ukawa na mawasiliano naye na awe ni mtu unayemuamini.  Mfuatilie kwa karibu na wala usimuache akajichunga mwenyewe. Najua unaweza ukawa unamuamini lakini kujiaminisha zaidi siyo mbaya.
Nasema hivi kwa kuwa, sote tunajua siku za sikukuu zinavyokuwa. Ni siku ambazo hata wale ambao hawakuwa na mawazo ya kusaliti wanajikuta wakifanya hivyo.
Wapo ambao walitoka wakiwa wazima lakini wakashawishika kunywa pombe na wakafanya ambayo hawakudhamiria. Zungumza naye mara kwa mara na mkumbushe umuhimu wa yeye kujichunga na kutokusaliti kwa kuwa uko mbali naye.
Muwekee mipaka
Si vibaya pia ukamuwekea masharti na mipaka kwa siku hiyo. Kwa mfano unaweza kumkataza pia asitoke ikishafika saa moja. Awe nyumbani na wewe uwe nyumbani, muutumie muda huo kuzungumza mambo mengi ambayo yatawaliwaza.
Pia suala la pombe unaweza kumtaka asinywe hata akiwa yuko nyumbani. Hivi utajisikiaje pale ambapo utampigia simu mpenzi wako na yeye akakuambia yuko nyumbani, amekunywa pombe na amelewa sana?
Hata kama amelewa akiwa nyumbani lakini haileti picha nzuri. Sote tunajua madhara ya pombe kwa hiyo ni vizuri tukashauriana kutotumia kilevi hicho.

Mfanyie ‘sapraizi’
Zaidi ya yote, kuna kitu kinaitwa ‘sapraiz’. Kwa lugha ya kawaida neno hili linamaanisha kumfanyia mtu kitu ambacho hakukitarajia. Katika siku za sikukuu wengi wamekuwa wakiwafanyia wapenzi wao ‘sapraiz’ lakini kwa yule ambaye yuko mbali na mpenzi wake ‘sapraiz’ kubwa unayoweza kumfanyia ni kumtembelea.
Hebu jiulize, wewe uko Mwanza na mchumba au mpenzi wako yupo Dar. Mmekuwa mkiwasiliana na akakueleza kuwa, kutokana na kubanwa na mambo hataweza kufika huku na wewe pia ukiwa huwezi kumfuata.
Kutokana na mazingira hayo, mnaendelea kuwasiliana lakini siku moja kabla ya sikukuu, ukijua kabisa yeye atakuwa nyumbani, unapanda gari na kwenda Dar kisha ukifika unampigia simu na kumwambia aje akupokee stendi.
Kwanza hataamini kile unachomwambia lakini akishakuona hiyo furaha yake haiwezi kuelezeka. Wapo waliofanikiwa kufanya ‘sapraiz’ hizo na wameona jinsi walivyowafurahisha wapenzi wao.
Naomba kwa kumalizia niseme tu kwamba, hakuna kitu kinachouma kama kusherehekea sikukuu huku mpenzi wako akiwa mbali na wewe. Utakuwa ukiumia zaidi pale utakapowaona wenzako wakitoka na wenza wao huku wewe ukiwa mpweke.
Lakini kwa kuwa hiyo yote ni sehemu ya maisha, huna sababu ya kuumia sana. Kwa kufanya hayo niliyoyaeleza hapo juu, angalau utapata faraja na naamini siku itapita na maisha mengine yataendelea kuwepo.
Kikubwa ni kuombeana uzima na kila siku kumuomba Mungu uhusiano wenu uwe ni wenye kutawaliwa na furaha na amani. Wazungu wanasema; Where there is true love, distance doesn’t matter, wakimaanisha kwamba penye penzi la dhati na la kweli, umbali siyo tatizo.

 Niishie hapo kwa leo, niwatakie maandalizi mema ya Sikukuu ya Idd.
back to top