WOLPER, KUWAJALI WAZAZI SIYO FEDHA,,,

No Comments
NINAMFAHAMU Jacqueline Wolper, kama mmoja wa mastaa wa filamu za Kibongo. Anajitahidi kuigiza na muonekano wa mwili wake unamsaidia sana kuvutia mashabiki. 

Siku kadhaa nyuma, niliwahi kuwa mmoja wa waandishi waliokuwa wakifanya naye mahojiano maalum ofisini kwetu.
Anajua kujieleza na ni mtulivu katika kujibu maswali anayoulizwa, huenda kwa vile anajua athari za maneno ya haraka, yasiyoeleweka na yaliyo na utata. Kwa hilo nilimpenda sana. Katika siku hiyo, licha ya mambo mengi aliyoeleza, hasa jinsi alivyoanza uhusiano wa kimapenzi na mpenzi wake wa zamani, Dallas lakini pia aliwazungumzia wazazi wake, aliodai wanaishi Kibaha.
Alisema ni wazazi wanaojimudu kimaisha, kwa maana kwamba maisha ya kawaida hayawasumbui, wanakula wanachohitaji, wanapata kinachotakiwa na watoto wanakwenda shule, kama alivyosomeshwa kiasi chake Jacqueline.
Nimewahi kuona filamu zake kadhaa alizocheza. Ni muigizaji mzuri, lakini angekuwa mzuri zaidi kama angepata muongozaji mahiri katika kisa cha kusisimua. Pamoja na uzuri wake, ubovu wa ubora wa filamu za Kibongo kwa ujumla wake unamfanya kuangukia katika shimo lile lile, la udhaifu wa hadithi, uhalisia wa kinachoigizwa na kushindwa kuendana na wakati katika tukio husika.
Katika siku za karibuni kumekuwa na madai mengi dhidi yake, hasa juu ya kile wanachodai, kushindwa kuwatunza wazazi wake. Huenda alishindwa kuvumilia jambo hilo, au alichoka na wanaodai hivyo, kiasi cha kuamua kuwajibu. Kama walivyo mastaa wengi, alifanya hivyo kupitia mtandaoni.
Haya ndiyo niliyoyakuta, yakidaiwa kuandikwa naye. “Wazazi wangu ni matajiri sana, kwa pesa gani nyingi nilizonazo za kuwafikia wao kiasi cha kuwapa matunzo??? Bado nawategemea hivyo wanaodai nimetelekeza wazazi ni waongo tu.”
Ni kauli inayoonyesha kwa kiasi gani alichukia. Nadhani hata mimi ningechukia kama ningeambiwa maneno hayo, kwa sababu najua kila mmoja wetu anawapenda wazazi wake na kwa ajili hiyo, atafanya kila analoweza kuhakikisha anawatunza vizuri.
Nilijaribu kupiga namba yake mara kadhaa ili niweze kupata ufafanuzi zaidi wa kauli yake, lakini bahati mbaya hakupokea hata baada ya kumtumia ujumbe mfupi wa maneno kujitambulisha. Sikujali.
Kilichonipa ukakasi ni aina ya maneno aliyosema.
Wazazi wake ni matajiri sana? Huenda kweli wanazo na kama hivyo ndivyo, nadhani yeye ni staa pekee aliyeingia katika uigizaji akitokea kwa wenye nazo, maana kumbukumbu zangu zinanionyesha wengi walijiingiza katika sanaa ili kusaka mkwanja wa kuwakwamua wao na wazazi wao!
Ninachotaka kumwambia Jacqueline ni kwamba matunzo ya wazazi ni zaidi ya fedha. Pesa ni maua ambayo hunyauka. Leo unaweza kuwa nazo na kesho zikapotea.
Watu wengi huamini kuwatunza wazazi ni kuwapa fedha ili watatue matatizo yao mbalimbali yanayowakabili.
Fikra hizi siyo sawa. Wazazi, hata wawe hohehahe kiasi gani, wanahitaji upendo zaidi ya vitu hivi. Wanahitaji mtoto anayewajali na kuwasikiliza. Unaweza kumpa mzazi wako kila kitu, lakini bado akawa hana furaha na wewe kwa sababu hujali na kusikiliza anachokisema.
Kama unawapa wazazi wako kila kitu lakini ukawa huwasikilizi wanapokuambia uvae mavazi ya heshima mbele ya kadamnasi ni kazi bure. Wakisema hawapendi tabia yako ya kubadilisha wanaume na wewe ukawa umeziba masikio ni sawa na hakuna.
Wolper na mastaa wengine, mashabiki wenu wanategemea muwe na kitu cha ziada mbele ya familia zenu. Kitu cha muhimu zaidi kwa wazazi wetu ni heshima, utii na kuwajali!
back to top