
Rais Jakaya Mrisho
Kikwete alipotembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa
ya Fahamu (MOI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jana (Jumamosi)
kuwajulia hali
wanahabari wawili – Ndugu Salum Mkambala wa Channel Ten
(juu) na (chini) Ndugu Margaret Chambiri wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC). (picha: Freddy Maro/IKULU).
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Gazeti la Mwananchi la leo, Jumapili, Machi 9, 2014, kwenye ukurasa wake wa tano, limechapisha habari zenye kichwa cha habari –“JK awatembelea Maranda, Mkambala Hospitali ya Taifa Muhimbili.”
Katika
habari hiyo, Gazeti hilo limeripoti: “Rais Jakaya Kikwete jana
alimtembelea mfungwa, Rajab Maranda anayetumikia kifungo cha miaka 18
gerezani kwa wizi wa fedha za Akaunti
ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aliyelazwa
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akisumbuliwa na tatizo la mgongo.”
Habari
hizi ni uongo. Mhe. Rais hakumtembelea Ndugu Maranda jana (Jumamosi)
kama ilivyoripotiwa na gazeti hili na wala hajawahi kumtembelea siku
yoyote iwe ni hospitalini ama kwingineko. Kwa hakika, ni jambo la
kusikitisha kuwa Gazeti lenye heshima na hadhi kama Mwananchi linaweza kujiingiza katika utunzi na uandishi wa uongo wa kiasi hiki.

Ukweli wa mambo yaliyotokea jana ni kama ifuatavyo:
Ni
kweli Mhe. Rais alitembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa
Mishipa ya Fahamu (MOI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jana
(Jumamosi). Alikwenda kuwajulisha hali wanahabari wawili – Ndugu Salum
Mkambala wa Channel Ten na Margaret Chambili wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC).
Mhe.
Rais alianza kumtembelea Ndugu Mkambala ambaye amelazwa wodi binafsi
–Private Ward – D, kufuatia ajali ya gari iliyomfika kwenye eneo la
Visiga, Mkoa wa Pwani, akiwa njiani kwenda Morogoro mwishoni mwa wiki.
Chumba hicho kilikuwa na wagonjwa watatu.
Baada
ya kuzungumza na Mkambala, Mhe. Rais, kama ilivyo kawaida yake
anapotembelea wagonjwa hospitali, aliwasalimia na kuwajulia hali
wagonjwa wengine wawili ambao wako katika chumba hicho kimoja na Ndugu
Mkambala.
Wagonjwa hao wawili ni Ndugu John Mhina, ambaye huko nyuma alipata kusoma na Mhe. Rais na Ndugu Reuben Nyanga.
Baada
ya kumaliza kuwajulisha wagonjwa hao wa Private Ward D, Mhe. Rais
alikwenda kwenye wodi nyingine binafsi – Private Ward K – ambako
alimjulia hali Ndugu Margaret Chambiri ambaye ni mgonjwa pekee
aliyelazwa katika chumba hicho. Baada ya hapo, Rais Kikwete aliondoka
Muhimbili kurudi Ikulu, Dar Es Salaam.
Hakuna wakati wowote, Mh. Rais alimtembelea Ndugu Maranda ama mgonjwa mwingine kwenye Hospitali hiyo ya Muhimbili.
Ni
matarajio ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, kuwa Gazeti la
Mwananchi na wahariri wake, watakuwa wakweli kwa nafsi zao wenyewe na
watakuwa na busara ya kutosha kusahihisha makosa haya kwa misingi ya
taaluma ya uandishi wa habari ambayo ni dhahiri wanaijua fika.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
09 Machi, 2014