HATA KAMA NI MLEVI, MPENDA ‘TOTOZI’, MPE MUDA WA KUBADILIKA!


KATIKA safari ya maisha, yapo tunayokutana nayo ambayo wakati mwingine yanatukatisha tamaa lakini kikubwa kinachotakiwa ni ujasiri wa kukabiliana nayo na kuyaacha maisha yaendelee kuwepo.
 Naomba niseme tu kwamba wapo wanawake ambao ni jasiri sana. Ujasiri ninaouzungumzia hapa ni ule wa kuwa na moyo wa kukabiliana na wanaume wenye tabia za ajabu kupitiliza.

Unamkuta msichana kaolewa na mwanaume chapombe kupita maelezo lakini anamvumilia, anakuwa ndiye wa kumfulia nguo zake hata zenye matapishi, anamfungulia mlango usiku wa manane lakini kesho yake anaomba tena kwa lugha ya kimahaba akimtaka mumewe apunguze ulevi na awahi kurudi nyumbani. Wanawake hao wapo huko mtaani.
Wapo wanawake ambao waume zao au wapenzi wao ni viwembe, wanajulikana kwa kupenda visichana lakini utakuta mke akipelekewa taarifa kuwa mumewe kaonekana maeneo f’lani na kibinti anapuuza kisha anafuatilia kimyakimya.
Lakini wapo ambao kila siku wanawafumania wapenzi wao na kwa kuwa wana mapenzi ya dhati kwao na hawako tayari kuwakosa, wanavumilia huku wakihangaika kutafuta tiba ya tatizo, huo ndiyo tunaouita uvumilivu.
Siyo unakuwa mvumilivu kwa mumeo kuchelewa kurudi kutoka kazini, hapana! Unamvumilia mwanaume ambaye unajua wazi muda huu kishatoka kazini, yuko maeneo f’lani anapata masanga na marafiki.
Ukiweza kumvumilia huyo kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja ndani ya ndoa hadi tabia hiyo ikapungua au akaiacha kabisa, wewe ndiye mwanamke jasiri.
Mpenzi msomaji wangu, tukumbuke ule msemo wa Kiswahili usemao mvumilivu hula mbivu. Wapo ambao walikuwa na uchu wa kufanikiwa lakini kwa kuwa muda wao ulikuwa bado, waliishi maisha ya tabu sana. Walivumilia na leo wanayafurahia maisha.
Hili lipo hata katika maisha ya kimapenzi. Uvumilivu una nafasi kubwa sana kiasi kwamba usipokuwa na subira, unaweza kukosa furaha ambayo Mungu amekupangia.
Umetokea kumpenda mtu f’lani lakini kwa bahati mbaya ukakutana na tabia ambazo hukuzitarajia, suluhisho haliwezi kuwa ni kumuacha, ukimuacha wenzako watamchukua, watambadilisha kisha wataishi maisha ya raha huku wewe ukibaki ukiumia na kusema; ‘yule alikuwa wangu, sijui kwa nini nilimuacha’.
Umekutana na mwanaume mlevi kupindukia ambaye bila kufika saa sita usiku hajarudi nyumbani au mwanaume ambaye asione ‘sketi’ ikikatiza mbele yake lakini moyoni mwako ukawa na imani kwamba ndiye mwanaume wa maisha yako, usikurupuke kumuacha, kufanya hivyo yaweza kuwa ni kuipiga teke bahati yako.
Kama huamini katika hili, jaribu kuchunguza na utabaini wengi ambao sasa hivi wanaishi maisha ya furaha na amani walivumiliana kwa mengi hadi kufikia hatua uhusiano wao ukasimama. Kuwa na subira na wala usiwe ni mtu wa kukata tamaa haraka.
Katika maisha ya sasa, watu wamekuwa hawaeleweki, hakuna unayeweza kuwa na uhakika naye asilimia mia moja kuwa anakupenda kwa dhati, subira yako ndiyo itakufanya ugundue hilo.
Mvumilie mpenzi wako huku ukijaribu mara kwa mara kuzungumza naye, usiwe mwepesi wa kuchukua uamuzi ambao unaweza kuja kuujutia kama ambavyo inawatokea baadhi ya watu sasa.
Ndiyo maana hata wiki iliyopita nilisema, huna sababu ya kubadili wapenzi kila baada ya muda na hiyo itatokea tu kama utakuwa ni mvumilivu kwa mtu ambaye utatokea kumpenda.
Kwa mfano leo utakutana na mpenzi ambaye hakupi ile furaha ya faragha uliyotarajia labda kutokana na kutokuwa na nguvu za kiume au maumbile yake ni madogo sana. Je katika mazingira hayo utamuacha? Huo nao ni mtihani mwingine.
Nasema ni mtihani kwa kuwa, mwanamke anaweza kushindwa kuvumilia huku akijiuliza kwenye ndoa wataishije bila kupeana yale mambo. Lakini mimi nawaambia wapo watu walivumilia hayo pia na Mungu akaleta baraka zake, mabadiliko yakaonekana na watu wakaendelea na maisha yao.
Mimi nadhani unapotokea kumpenda mtu kwa dhati kabisa, kuwa tayari kukabiliana na changamoto zote utakazokutana nazo. Yapo mengine yanaweza kujitokeza ambayo Mungu anaweza kuwa anakupa mtihani ni kukupima imani yako na ndiyo maana tunakumbushana kuwa wavumilivu.

Ni hayo tu kwa leo, 
back to top