DULLY ACHA KULALAMA, NENDA KITANZANIA ZAIDI

Dully Sykes.
MWANZONI mwa miaka ya 2000, aliibuka kijana mmoja hivi mitaa ya Kariakoo, jijini Dar akiitwa Dully Sykes, akiwa miongoni mwa maelfu ya vijana wa Kibongo waliopania kujiajiri kupitia muziki wa kizazi kipya, Bongo Fleva.

Dully alianza ‘game’ vizuri na ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba tokea alipoanza hadi sasa ameendelea kuwa katika matawi ya juu, licha ya vijana wengi kuingia na kung’ara katika fani hii ambayo sasa, licha ya kupunjwa na wajanja wachache, ni moja ya ajira binafsi za uhakika zinazowafanya wengi kuendesha maisha kitajiri.
Miongoni mwa nyimbo zilizompa umaarufu mkubwa, kiasi cha baadaye kuja kujipatia jina la utani la Mr Misifa, ni pamoja na Julieta, Nyambizi na Hi!
Dully ni mpenda sifa kweli. Ni mtu ambaye anapenda uwepo wake kujulikana, ingawa binafsi, sijawahi kumuona kama mpenda sifa za kijinga, ana utani mwingi, kwa sababu ni mcheshi na mwenye majigambo ya watoto wa mjini, lakini kwa wanaomjua!
Mimi ni shabiki wake mkubwa, kwa sababu anachojali yeye ni watu kufurahi kwa muziki wake, hajali kama kuna ujumbe wowote anautoa kwa jamii inayomzunguka au la na zipo nyimbo kadhaa zinazoweza kuthibitisha hili. Anapenda watu warukeruke sana na kwa hilo nadhani amefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu ameamua kuwa na aina yake ya uimbaji.
Hivi karibuni Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) chombo cha serikali chenye wajibu wa pamoja na mambo mengine, kulinda maadili ya Kitanzania katika sanaa, lilizuia kuendelea kuchezwa kwa video ya wimbo wake uitwao Kabinti Special kwa madai kwamba ulifanywa kinyume na maadili yetu kama taifa.
Mimi nimeiona video hiyo, niwe mkweli kwamba ni moja kati ya video kali, za kisasa, kama vile za wale mastaa wa Visiwa vya Carribean. Imetulia kweli kwa vijana wa kisasa, hasa hawa wa Dot.com.
Kwangu tatizo liko moja tu, jinsi yule Video Queen wake alivyovaa na kucheza. Siyo kabisa, ni kachupi tu na hivyo vimbwanga vingine ni hatari, achilia mbali Diamond kuvaa fulana yenye kuwatukana polisi kwa maneno ya Kiingereza yasemayo Fuck the Police!
Nimesema mara nyingi, msanii, awe wa filamu au muziki, anapojiachia yeye mwenyewe au wacheza shoo wake kwa nguo za nusu utupu, ni dalili za kuishiwa uwezo wa kufanya kazi, hivyo anachofanya ni kuwapumbaza watu watazame kwa matamanio utupu wa wasichana badala ya umakini wa kazi anayoitazama!
Siku zote nimekuwa muumini mkubwa wa ulinzi wa utamaduni wetu, kwa sababu kadiri siku zinavyokwenda, yaonekana wazi tunataka kuuondoa utamaduni wetu na kwenda kuubwaga Ulaya bila sababu zozote za msingi. Baadhi ya wasanii wetu wanadhani ili kazi zao ziwe bora ni lazima wafanye mambo kama ya kina P Diddy, 50 Cent au Justin Bieber. Wanasahau kwamba wao ndiyo mabalozi wa utamaduni wetu.
Siyo Dully peke yake, kuna vijana wengi wa Bongo Fleva wanaoleta ujinga wa kukataa utamaduni wao na kudhani kuwa kuvaa nusu utupu ni kwenda na wakati. Zipo nguo nzuri tu ambazo kama tutawatumia wabunifu wetu wa mavazi, tunaweza kufanya vizuri sana katika soko la kimataifa.
Kuna binti mmoja wa Kitanzania aliitwa Renee Ramila, sijui yuko wapi hivi sasa.
 Licha ya historia kusema aliishi Ulaya, lakini alirejea nyumbani na kufanya bonge la wimbo, ukiitwa Ngoma za kwetu, akivaa kitamaduni na akicheza kwa namna ambayo alijizolea mashabiki wengi na mara kadhaa, alialikwa kufanya shoo katika Tuzo za Kola kule Afrika Kusini.

Kiafrika zaidi, drop down your comment kuboresha utanzania zaidi...
back to top