
Tunakutana tena katika safu yetu hii ya ujasiriamali ambayo ingawa walengwa ni wanafunzi, lakini hata watu wazima pia inaweza kuwasaidia kwa kuwa hakuna umri wa mwisho katika kutafuta maisha bora.
Wapo watu ambao wamekuwa kati ka biashara kwa muda mrefu lakini bado hawajaona faida yoyote kiasi cha kuwafanya waanze kuchanganyikiwa.
Jibu ni rahisi. Wanachopaswa kukiweka akilini mwao ni kuachana na mawazo ya kukunua bidhaa zinazozalishwa na kampuni, lakini badala yake, wafikirie kuinunua kampuni inayozalisha bidhaa hizo.
Na katika kufikiria kuinunua kampuni, ni lazima pia uwezo mkubwa kifedha utahusika. Matajiri wote duniani ni watu wanaoamini sana katika kuweka akiba na kuwekeza. Ni watu ambao huwekeza katika miradi au akiba katika mabenki kiasi cha asilimia kati ya 27 hadi 30 ya mapato yao.
Utajiri unatokana na jinsi unavyovumilia maumivu ya kuondokana na utumwa wa kifedha na mabadiliko ya tabia yako katika matumizi ya fedha. Maana hasa ya usemi huu ni kwamba kuna muunganiko wa vitu vingi vinavyomuongoza mtu kuondokana na umasikini na kujikuta akiwa na hali nzuri kifedha.
Jambo lingine linaloweza kukusaidia ni kujifunza kutokana na mafanikio ya wengine. Wapo baadhi yetu ambao tunawatambua watu waliofanikiwa mbele ya macho yetu. Yaani mafanikio yao yameanza huku tukiwaona, walianza na genge la nyanya, likapanuka na kuwa duka la vyakula, kabla ya kuona wakifungua viwanda vidogo vya usindikaji wa vyakula.
Ni lazima kuwa na tabia ya kujifunza njia nzuri kutoka kwa wengine na kuachana na watu ambao vitendo vyao havikuongozi katika mafanikio. Jitengeneze katika namna ambayo unataka kuwa.
Utajikuta kwamba kwa kuwekeza katika nafsi yako kwanza, fedha zitaanza kuingia katika maisha yako. Maisha yako yanatakiwa kuwa kwa namna hiyo huku ukijijengea jeshi lako la mtu mmoja kwa kuweka akiba ya fedha zako kwa ajili ya kukufanyia kazi.
Hata hivyo, wako watu wanaoamini kuwa fedha siyo suluhisho la kila kitu katika maisha. Pesa zaidi haziwezi kumaliza matatizo yako. Wataalamu wanasema fedha ni kama kioo, kinachoyaleta maisha yako katika mwanga uonyeshao tabia zako halisi.
Kama mtu hana uwezo wa kuhimili kazi yenye malipo ya shilingi milioni 18 kwa mwaka, kitu kibaya kinaweza kumtokea endapo ataweza kupata malipo ya zaidi.
Pesa zaidi zinaweza kummaliza. Watu wanaopata kiasi cha shilingi milioni 100 kwa mwaka huwa na matumizi mabaya, hasa kama hawana weledi wa kutosha juu ya fedha.
Wazazi ni muhimu katika maisha yako. Ni watu ambao wanaweza kukupa mwanga. Kama unataka kuishi tofauti na maisha ya wazazi wako, basi hakikisha haufanyi vitu vyote ambavyo vilikuwa vikifanywa na wazazi wako.
Ni lazima kuachana na maisha ya kizazi kilichopita kama unataka kuwa na aina tofauti ya maisha.