WIKI hii nitazungumzia suala la kazi linavyochukuliwa kama kigezo muhimu kwa walio wengi kabla ya kuoa ama kuolewa. Ni kitu cha kawaida mwanaume anapomtamkia msichana kwamba anataka kumuoa, swali la kwanza litakuwa je, unafanya kazi gani?
Licha ya kwamba mara nyingi wanawake ndiyo wamekuwa wa kwanza kudadisi juu ya hilo, sasa hivi baadhi ya wanaume nao huchunguza kwamba wale ambao wamewapenda wanafanya kazi au hawafanyi.
Kwa hali ilivyo sasa, kazi imekuwa ni kigezo cha msingi sana ili ndoa ziweze kuwepo. Hata hivyo, wakati wengine wakijitahidi kutafuta wachumba wanaofanya kazi, wapo wanaume wasiopenda kuoa wanawake wanaofanya kazi huku wakitoa sababu ambazo kwa kiasi kikubwa hazina uzito bali ni imani potofu tu walizonazo.
Huko nyuma wanawake walikuwa wakichukuliwa kama mama wa nyumbani tu wasiostahili kufanya kazi nje ya nyumba. Wao walionekana ni viumbe wanaostahili kufanya kazi za nyumbani kama vile kuosha vyombo, kufua, kupika,kulea watoto na zaidi ya yote kuwastarehesha waume zao.
Dhana hiyo katika kipindi hicho iliwaathiri wanaume wengi na baadhi kujikuta wakikataa kuoa wanawake wanaofanya kazi. Hata ikitokea kumpenda mwanamke anayefanya kazi, atamshauri kuacha ili amuoe.
Mawazo hayo mpaka sasa yapo kwani wapo wanaume wasiotaka kuoa wanawake wanaofanya kazi huku kila mtu akitoa sababu zake.
Si hivyo tu, dhana hii pia imewaathiri wanawake walio wengi, baadhi hawataki kabisa kufanya kazi huku wakibweteka wakiamini wataolewa na wanaume wanaofanya kazi na kuyafurahia maisha.
Mimi siwezi kuyaingilia maamuzi ya mtu ila ni vizuri tukashauriana katika mambo ambayo ni yenye manufaa kwetu.
Ifahamike kwamba, wanawake pia wana haki ya kufanya kazi, hawakuumbwa kwa ajili ya kukaa nyumbani tu na kuwategemea waume zao kwa kila kitu.
Kwa hali ilivyo sasa, wanaume kwanza wamekuwa makini sana kiasi kwamba kabla hawajachukua uamuzi wa kuoa wanahakikisha wana kazi ambayo itawafanya waweze kuendesha maisha vizuri ndani ya familia. Naamini hakuna mwanaume anayeweza kudiriki kuoa huku akiwa hana kazi na ikitokea hivyo basi mwanaume huyo atakuwa na matatizo.
Wapo wanaume ambao, licha ya kuwa na kazi lakini pia wanapooa mwanamke ambaye hana kazi hujitahidi kuwatafutia kibarua angalau wasaidiane kuboresha maisha yao. Hata hivyo, wanawake wengi sasa hawataki kabisa kuwa tegemezi kwa waume zao na wamekuwa wakipigania haki sawa na hivyo wengi wao wamekuwa wakikataa ile dhana ya mwanamke ni mama wa nyumbani.
Cha kufurahisha ni kwamba, hivi sasa ukiingia kwenye maofisi mbalimbali, utakuta wanawake wengi wakiwa katika nafasi za juu tena wengine wakiwa mabosi wa wanaume.
Lakini sasa, kila kitu kinakuwa na hasara na faida zake.Tunapozungumzia faida za wanandoa wote kufanya kazi, kwanza tunadhihirisha usawa uliopo baina ya mke na mume kwamba wote wanastahili kufanya kazi na kuchangia katika maendeleo ya familia na ya taifa kwa ujumla.
Zaidi ya yote, wanandoa wanaweza kusaidiana katika kuchangia matumizi ya ndani ya familia kutokana na kila mtu kuwa na kipato. Maisha ya sasa ni kusaidiana na si kumtegemea mmoja, labda ziwepo sababu za msingi za mume kutegemea kipato cha mke ama mke kutegemea kipato cha mume.
Tunapogeukia katika upande wa pili, tunaweza kukutana na hasara ambazo zinaweza kupatikana kwa wawili kuoana wote wakiwa wanafanya kazi.
Utafiti umebaini kuwa, ni wanandoa wachache sana wanaofanya kazi na wanafurahia maisha yao ya ndoa. Baadhi wamekuwa wakishambuliwa na misuguano ya hapa na pale hali inayosababisha mazingira ya shari ndani ya nyumba.
Baadhi ya wanaume wanaeleza kwamba, kuoa mwanamke anayefanya kazi kunaweza kukukosesha heshima ambayo mwanaume anastahili kuipata kutoka kwa mke wake kutokana na kwamba, mwanamke anapokuwa na uwezo wa kupata kila kitu anachotaka bila kupewa msaada kutoka kwa mumewe kama ilivyojengeka, inaweza kusababisha kushuka kwa heshima.
Cha msingi kwa wanandoa wote ni kufahamu kwamba ndoa ni heshima na ili heshima hiyo idumu milele, lazima kuwepo na ushirikiano, uaminifu, maelewano na majukumu kwa kila mtu.
Tukumbuke ndoa siku zote ni makubaliano baina ya wawili waliotokea kupendana. Kwa maana hiyo hata mkioana wote mkiwa hamna kazi ni sawa na hakuna anayeweza kawaingilia.
Kwa kumalizia niseme tu kwamba, kazi ndiyo msingi wa maisha. Usipokuwa na kazi ni vigumu sana kuweza kupata pesa na usipokuwa na pesa hustahili kuzungumzia suala la ndoa hasa kwa mwanaume ambaye ndiye anayestahili kulipa mahari na pia kubeba jukumu la kumtunza mke na familia kwa ujumla.

Mawazo hayo mpaka sasa yapo kwani wapo wanaume wasiotaka kuoa wanawake wanaofanya kazi huku kila mtu akitoa sababu zake.
Mimi siwezi kuyaingilia maamuzi ya mtu ila ni vizuri tukashauriana katika mambo ambayo ni yenye manufaa kwetu.
Lakini sasa, kila kitu kinakuwa na hasara na faida zake.Tunapozungumzia faida za wanandoa wote kufanya kazi, kwanza tunadhihirisha usawa uliopo baina ya mke na mume kwamba wote wanastahili kufanya kazi na kuchangia katika maendeleo ya familia na ya taifa kwa ujumla.
Tunapogeukia katika upande wa pili, tunaweza kukutana na hasara ambazo zinaweza kupatikana kwa wawili kuoana wote wakiwa wanafanya kazi.