KWA NINI WATU WENGI HAWAFANIKIWI MAISHANI?

Kwa pamoja, nataka tuangalie kwa nini watu wengi hawafanikiwi katika ujasiriamali au katika maisha yao. Kuna sababu nyingi kwa nini wengi hushindwa maishani lakini sababu kuu ya msingi, huwa ni kukosa maarifa na ufahamu wa kufanya biashara au ajira katika kiwango cha juu kadiri
iwezekanavyo.
Kama uko kwenye chumba chenye giza, na hujui swichi ya kuwashia taa ilipo, hata ungepiga mayowe kiasi gani taa haiwezi kuwaka. Bali kama unajua swichi ilipo, hata mtoto wa miaka mitano anaweza kuigusa, taa ikawaka na nuru ikatokea mara moja.
Kwa hiyo kama uko kwenye chumba chenye giza, kazi yako kuu inatakiwa iwe moja tu - kutafuta swichi ilipo mpaka uipate. Hiyo ndiyo hekima inayoweza kumtoa mtu gizani mpaka nuruni.
Mchekeshaji Masanja Mkandamizaji alinisimulia mkasa mmoja uliompata dereva teksi mmoja hapa jijini Dar es Salaam unaofafanua kile ninachokisema hapa.
Anasema siku moja dereva teksi mmoja akiwa na abiria wake muhimu sana, alizimikiwa na gari yake ghafla. Akawa ameghafirika na hajui afanye nini lakini baada ya dakika kadhaa, akili yake ilitulia, akaamua aanze mwenyewe kuchunguza tatizo lilikuwa ni nini.
Baada ya nusu saa kupita, dereva teksi huyu hakupata mafanikio na kijasho chembamba kilianza kumtoka. Kwa hofu na mashaka, aliamua kumpigia simu fundi makenika mmoja bingwa aje kumsaidia.  Bahati nzuri yule fundi hakuwa mbali sana kutoka eneo lile na alikuwa ndiyo amemaliza kutoa huduma kwenye gari lingine lililokuwa limeharibika.
Yule fundi alipofika tu, moja kwa moja akaliangalia lile gari na ndani ya dakika tano akawa amegundua tatizo liko wapi. Akabadilisha kifuniko sehemu fulani, akapiga ‘stata’ na gari likawaka. Wakati akijifuta mikono tayari kwa ajili kuondoka, yule dereva teksi akauliza gharama ya ufundi.
“Shilingi elfu hamsini tu rafiki,” alijibu fundi makenika.
“Haa, yaani umekuja hapa, hata dakika tano hujamaliza umebadilisha tu kifuniko, halafu unadai shilingi elfu hamsini, kivipi ndugu?” alilalamika dereva teksi.
Yule fundi kwa utulivu na taratibu, alimuangalia yule dereva teksi halafu akasema maneno yafuatayo ya msingi sana ambayo ni somo na shule kwetu sote; “Kazi ya kubadilisha kifuniko, gharama yake ni shilingi 1000 tu lakini kazi ya kujua tatizo ni nini na liko wapi, gharama yake ni shilingi 49,000.”
Masanja aliponisimulia kisa hiki maeneo ya Mlimani City tulipokutana takriban wiki tatu zilizopita, nilicheka sana lakini pia nilipata ufunuo mwingine zaidi wa mafanikio hapa duniani, kwamba watu wengi ni maskini kwa sababu hawataabiki kutafuta kujua jinsi ya kuyawasha magari yao!
Watu wengi sana wamepaki magari yao yakiwa yamezimwa kando ya barabara kwa kuwa wamekata tamaa na hata wamesahau kuwapigia simu mafundi (wataalamu) waweze kuwasaidia. Na wengine hawako tayari kulipia elimu na maarifa ambayo yangewatoa sehemu moja na kuwapeleka sehemu inayofuata maishani.
Sasa zipo namna kadhaa za kuongeza maarifa ya ujasiriamali wako kwa haraka ambayo yatakusaidia kuongeza kasi ya kufanikiwa katika maisha yako. Kutokana na uzoefu wa mabadiliko ya maisha yangu binafsi, nimejifunza kwamba zipo mbinu tatu zenye uwezo wa kukupa maarifa na siri za kwenda mbele maishani.
Ya kwanza, ni kuchagua marafiki wanaokwenda kule unakotaka kwenda au wawe wameshafika tayari. Watu wengi wanapenda kufanikiwa lakini hawana marafiki waliofanikiwa. Hii ni ngumu sana. Huwezi kuwa unataka kuwa milionea lakini katika marafiki wote ulionao, hakuna hata mmoja tajiri. Ni kweli inawezekana lakini ni ngumu na itabidi ufanye kazi ya ziada.
Kanuni hii ni ya muhimu kwa kuwa kimsingi huwezi kuwa zaidi ya watu unaokuwa nao mara kwa mara. Lakini pia, mara nyingi hawa watu wanaokuzunguka mara nyingi ndiyo wavunja moyo nambari moja unapowashirikisha ndoto zako.
Kwa sababu wao wamekuzoea, huwa hawawezi kukuchukulia ‘serious’ unapoamua kufanya kitu kipya au cha tofauti. Kwa mfano ukisema, ‘jamani, mimi nimeanzisha biashara yangu, nipeni sapoti ya japo kuniungisha’, mara nyingi mioyoni mwao, wanaweza kusema, ‘yani na wewe, tangu lini umekuwa mfanyabishara?’ 
Wakati mwingine wanaweza kukuambia waziwazi au peupe kabisa.
Itaendelea wiki ijayo.

back to top