Ninapotazama mambo ya nchi yanavyokwenda kitotototo nasikitika; lakini kubwa zaidi naamini kuwa kuna baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali hawataki kuliona taifa hili likistawi na kunawiri katika amani na uchumi. Swali langu:
Tunawezaje kuliokoa taifa linaloongozwa na wenye nia mbaya?
Kwangu mimi taifa ni kitu cha kwanza kuliko rais, mawaziri, wabunge na waheshimiwa wa ngazi yoyote ile, hivyo siko tayari kuona masilahi ya nchi yanaachwa kwa lengo la kumlinda na kumtetea mtu fulani eti tu kwa sababu ni kigogo serikalini.
Kwangu mimi taifa ni kitu cha kwanza kuliko rais, mawaziri, wabunge na waheshimiwa wa ngazi yoyote ile, hivyo siko tayari kuona masilahi ya nchi yanaachwa kwa lengo la kumlinda na kumtetea mtu fulani eti tu kwa sababu ni kigogo serikalini.
Vipi sakata zito kama la IPTL linaweza kumalizwa kwa watu kuhojiwa wanaoafiki waseme ndiyo na wasioafiki waseme siyo na mwisho wa siku walioafiki washinde na mambo yaendelee kana kwamba hakuna tuhuma nzito kwenye jambo hilo?
Ninyi watu, ninyi viumbe wa Mungu, ninyi wenye mamlaka katika nchi hii!! Hivi kwa nini hadi karne hii tumeshindwa kujifunza namna ambavyo nchi inatakiwa kuongozwa kwa kufuata wajibu na mipaka ya mihimili inayotambulika katika nchi husika?
Sheria za nchi ziko wazi, kwamba mihimili inayotambulika ni mitatu ambayo ni serikali (kuongoza), mahakama (kutafsiri sheria), na bunge (kuisimamia na kuishauri serikali). Muongozo wa nchi umeweka wazi mipaka ya mihimili hii hata watoto wadogo wanajua!
Kinachonishangaza ni kuona namna serikali na bunge zinavyotaka kufanya kazi zote za mihilimi mitatu kwa wakati mmoja. Kwa mfano likitokea jambo lolote la jinai ambalo linaihusu serikali, utaona jinsi ambavyo chombo hicho kinataka kuongoza, kujishauri na pengine kutafsiri sheria kwa kuwafanya watuhumiwa fulani kuwa hawana hatia, kasoro hizo zinafanywa mara nyingi na bunge pia!
Sakata la IPTL kwa mfano hai, limeibuliwa na bunge kama msimamizi lakini wabunge wamekuwa wakishinikiza kuundwa kamati teule ili kupata nafasi za kuwahukumu baadhi ya watendaji. Jambo hili limefanywa na bunge katika kamati nyingi ikiwemo ile ya Oparasheni Tokomeza ambayo mwisho wa siku iliwahukumu mawaziri ambao mpaka leo wanalalamika kuonewa.
Huwezi kuwa na nchi imara yenye bunge la kuhukumu watu, huwezi pia kuwa na serikali yenye dola isiyojua mambo ya kifisadi na jinai yanayofanywa ndani ya utawala wake mpaka chombo kingine kije kifukue maovu na serikali ijivalishe nguo kwa kuwalinda watuhumiwa. Ni aibu!
Nilitarajia serikali ingekuwa ya kwanza kujua kuwa IPTL kuna fedha zimeliwa na kufanya kazi yake kama dola kisha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani wakatafsiriwe sheria ikiwezekana wafungwe; haya makelele ya wanaosema ndiyo ya nini kwenye utawala wa sheria? Serikali inagawa watu, inachonganisha watu kwa sababu haijui jukumu lake! Najizuia kufoka!
Leo hii kila kona nchi inaliwa, mara twiga hai kasafirishwa, tembo wanne wameuawa, mahindi ya msaada yameibwa, vifaa vya hospitali ya kijiji vimepotea, fedha za mishahara zimeliwa, yaani ni madudu tupu utadhani serikali ipo likizo na kwamba wananchi wameachwa yatima.
Ni wajibu wa serikali kujichunguza yenyewe na kuwawajibisha wanaohujumu uchumi bila kusubiri kuchokonolewa kama pweza, matokeo yake inatoka hadharani ikiwa utupu na kuchutama kuficha aibu! Nachochea tu!
