MWAKA WA 7 SASA, BADO MARAFIKI TU!

No Comments


LOVE & Life ndiyo kolamu inayotukutanisha marafiki kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali kuhusu uhusiano na maisha. Bila shaka kwa wadau wa kona hii, watakiri kuwa imewabadilisha sana.
Kama ndiyo mara ya kwanza kuanza kusoma hapa, napenda kukuhakikishia kuwa hutajutia badala yake utaendelea kujifunza mambo mapya kila siku ambayo yatabadili fikra zako kuhusu uhusiano.
Leo nataka kuzungumzia jambo muhimu sana, hasa kwa upande wa wasichana. Kuna baadhi ya wasichana wamekuwa kwenye mateso makali ya manyanyaso kutoka kwa wapenzi wao.
Wapo wengine ambao wamekaa kwa muda mrefu kwa mwanaume mmoja kama marafiki tu kwa lengo la kupanga maisha ya baadaye lakini ghafla mwisho mwanaume anabadilika.
Rafiki zangu kuna mambo ya muhimu sana kufahamu kuhusu jambo hilo. Kwa bahati mbaya sana, wanaume wa zama hizi wamejaa uongo. Si wakweli, ahadi nyingi hewa huku wakisukumwa zaidi na tamaa za mwili kuliko upendo wa kweli.
Utakuta msichana yupo na urafiki na mwanaume kwa zaidi ya miaka mitatu – marafiki tu! Mipango mingi, lakini mwisho wa yote, mwanaume anaamua kukaa pembeni na kumuacha msichana wa watu akiwa ameshapoteza muda wake.
URAFIKI
Kitaalam katika kuelekea ndoa kuna hatua za awali kwa wapenzi kuzipitia. Lazima kwanza urafiki, uchumba na baadaye kuingia kwenye ndoa. Hizi ni hatua ambazo lazima zipitiwe kwanza.
Hatua zenyewe zina vipindi vyake.
Katika hatua ya kwanza ya urafiki ni kipindi cha wenzi kuchunguzana tabia. Ni muda wa kufahamiana kwa undani kuhusu mambo mbalimbali ambayo ni muhimu kuyajua.
Kwa mfano, hapa wachumba watarajiwa wanatakiwa kujua kuhusu suala la historia za kila mmoja, kujuana mila za makabila wanayotoka.
Mijadala ya suala la imani za dini nk.
Kipindi hiki kwa kawaida, si zaidi ya mwaka mmoja au zaidi. Kama muda utakuwa umezidi sana, si zaidi ya miaka miwili. Hatua hii itawasogeza kuelekea kwenye uchumba.
VIPI URAFIKI WA MUDA MREFU?
Inategemea na sababu. Mfano kama watarajiwa au mmoja wao ni mwanafunzi (nazungumzia wa vyuo) wanaweza kuwa katika urafiki kwa muda mrefu zaidi, lakini si zaidi ya miaka mitatu.
Ndugu zangu, kuna tofauti kubwa kati ya urafiki na uchumba.
Ikiwa tayari mmeshakubaliana na mmeshachunguzana     vya kutosha, hata kama bado mnaendelea na masomo mnapaswa kuingia kwenye hatua nyingine ya uchumba.
Lazima uhusiano wenu sasa ufahamike na wazazi wa pande zote mbili na taratibu nyingine ziendelee, vinginevyo uhusiano wenu utakuwa wenye mashaka na si ajabu mwisho mwanamke akaachwa kwenye mataa!
TAMBUA UKWELI
Ikiwa anakupenda, ana sababu gani ya kubaki kwenye urafiki kwa muda mrefu? Anakuchunguza! Atagundua nini kipya ikiwa mmeshakuwa pamoja kwa zaidi ya miaka mitatu?
Wakati mwingine, mwanaume anaweza kuwa na mwanamke kwa lengo la kumfanya chombo cha starehe tu.
Wengine wanashindwa namna ya kuachana maana wameshakuwa kwenye urafiki kwa muda mrefu.
Atajifanya ametulia lakini kichwani anapanga namna ya kukuacha. Yaani anatafuta sababu taratibu, siku ukijichanganya tu, hapohapo unakuwa umeachwa!
YEYE YUKOJE?
Uko kwenye urafiki na mwanaume kwa zaidi ya miaka mitatu sasa? Kama ndivyo, hebu tulia na utafakari; yukoje? Angalia tabia zake. Anakuchukuliaje?
Uhusiano wenu upo wazi kiasi gani? Zipo dalili za msingi za kuangalia ili kujua kama yupo kwenye mstari au ana yake. Nafasi haitoshi kuelezea kwa sasa, wiki ijayo nitaanzia hapo, USIKOSE!
back to top