MMOJA wa wasichana wawili raia wa Uingereza waliomwagiwa tindikali na watu wawili ambao bado hawajajulikana mjini Zanzibar Agosti 7 mwaka jana, ameibuka na kuliambia gazeti la Daily Mail la nchini humo jinsi tukio hilo lilivyotokea.
Katie, ambaye mwili wake uliharibika kiasi cha asilimia 30 kutokana na tukio hilo, alikuwa na rafiki yake, Kirstie Trup ambao walikwenda Zanzibar kwa kazi za kujitolea kuwahudumia watoto yatima.
Akizungumzia tukio hilo, msichana huyo anayeishi Hampstead, Kaskazini ya London, alisema mara tu baada ya kumwagiwa, tindikali hiyo iliondoa sehemu kubwa ya ngozi yao kuanzia kidevuni hadi tumboni, kiasi cha kuwafanya waonekane weupe.
“Walikuwa wawili kwenye pikipiki, aliyekuwa amepanda nyuma, alituangalia na kutabasamu, halafu akachukua dumu na kutumwagia, Kirstie aliloa mwili mzima.”
Madaktari wanaomtibu wamesema msichana huyo angeweza kutoona tena kama asingekuwa amefumba macho wakati alipofanyiwa kitendo hicho.
Kate Gee.
Watu waliokuwa karibu na tukio hilo, waliwasaidia wasichana hao kwa kuwamwagia maji kuondoa ukali wa tindikali hiyo kabla ya kupelekwa hospitali, na baadaye kupanda ndege kwenda London kwa matibabu zaidi. Katie aliharibika ngozi yake usoni, mgongoni, mikononi, tumboni na miguuni.
Sikio lake moja limelazimika kutolewa baada ya kuharibika vibaya na madaktari wanafanya mpango wa kumwekea la bandia. Aidha, ili awe mzima kabisa, anatakiwa kufanyiwa tena upasuaji mara 15 zaidi.
“Zamani nilikuwa naogopa sana kila niliposikia kuhusu upasuaji, lakini sasa imekuwa ni sehemu ya maisha yangu, madaktari walitaka kunitoa ngozi yangu ya kichwa ili waiweke sehemu ya uso, lakini nimekataa kwa sababu kichwa change ndiyo sehemu pekee ambayo haikuguswa na tindikali,” alisema msichana huyo.
Wasichana hao wawili walimwagiwa tindikali hiyo wakati hali ya usalama kisiwani Zanzibar ilipochafuka kufuatia matukio mfululizo ya aina hiyo, kwani mwezi mmoja baadaye, padre mmoja wa kanisa katoliki, Anselmo Mwang’amba naye alifanyiwa kitendo hicho.