Hata hivyo, wale wanaopata kipato cha chini, wameondoa mawazo yao katika uwezekano wa kuwa mamilionea, wanaona ni jambo lisilowezekana. Lakini nawathibitishia kwamba uwezekano huo upo, tena mkubwa.
Ipo mishahara ambayo watu wanapata, ambayo kwa akili ya kawaida inakuaminisha kwamba ni ndoto ya mchana kuweza kujiwekea akiba kiasi cha kukupatia umilionea.
Lakini hakuna kitu kisichowezekana chini ya jua. Kitu cha msingi ni nia yenye kuambatana na vitendo, maana wapo watu wanakuwa na nia kila siku, lakini hawafanyi lolote kuelekea kwenye kutimiza nia yao.
Kwa kawaida, umri ni kitu muhimu sana katika kuelekea mafanikio yako. Na umri mzuri zaidi ni kuanza kuwekeza angalau katika miaka 30 ya ujana, vinginevyo ni mara chache kuweza kufanikiwa kwa kuanza kuwekeza katika miaka 50 na kuendelea.
Kwa wanaopata mishahara midogo, wanatakiwa kuweka angalau robo ya kipato chao halali. Kwa mfano, mfanyakazi wa ndani ambao sisi huwaita mahausigeli au mashambaboi, ambao ndiyo hulipwa mishahara midogo zaidi katika jamii ya Kitanzania, wanaweza kuwa mamilionea kama watakuwa na nia hiyo.
Na kwa watu wa aina hii, ni lazima wawe na mipango ya muda mrefu, kwanza ya kuweka akiba ya fedha zinazotokana na vipato vyao na pili ni kubuni aina ya mradi wa kufanya baada ya makusanyo ya akiba yao.
Kwa mfano, hausigeli anayelipwa mshahara wa 20,000 anaweza kuweka hata nusu ya pato lake kwa mwezi, hasa kwa vile tunatambua kwamba wasaidizi wengi wa ndani hula na kulala kwa matajiri zao, hivyo suala la kodi ya nyumba, chakula na wakati mwingine hata mavazi huwa siyo la mfanyakazi.
Kama atafanya hivyo kwa mwaka mmoja, ni kuwa atakuwa na kipato cha shilingi 200,000. Hizi zinaweza kuwa zisimtoshe na anaweza akawekeza tena kwa mwaka unaofuata na kujikuta baada ya miaka yake miwili ya kujinyima, sasa anacho kiasi cha shilingi 400,000.
Fedha hizi zinatosha kuanzisha mradi mdogo unaoweza kumuongezea mtaji wake kila siku kama vile kuuza mihogo ya kuchoma au kukaanga na kuuza samaki, kuuza karanga au hata matunda ya msimu kama embe, machungwa, matikitimaji na kadhalika.
Kama nia ya mtu kama huyu ni kuufikia umilionea, mwaka mmoja baadaye, kwa vyovyote akiba yake benki inaweza kusomeka hadi zaidi ya shilingi laki tano, jambo litakalomaanisha kuwa mwaka unaofuata, mafanikio yanakuwa mara mbili au tatu.
Kitu cha msingi kabisa kutambua kwa mtu anayeusaka umilionea kwa kuanzia na mtaji mdogo ni kuamini katika kujibana, ikibidi kuachana na matumizi yoyote yasiyo ya lazima.
Vitu vingine vinavyopaswa kufanywa na mtu asakaye umilionea ni kununua vyakula vya jumla ambavyo huuzwa kwa bei rahisi tofauti na rejareja. Na ukishanunua vyakula hivyo, hakikisha hauli chakula tofauti na ulichohifadhi hadi akiba yako iishe.
Msaka umilionea pia hana budi kupunguza gharama za usafiri, hana sababu ya kupanda pikipiki au Bajaj kwenda sehemu ambako daladala hufika na kwa wale wenye vyombo vya usafiri, kama magari, wanapaswa kuchagua yale yasiyokula sana mafuta.
Pia ni lazima wajitahidi kuepuka kupanga nyumba zenye gharama kubwa, ni vizuri kuhamia sehemu ambako kodi yake ni ndogo.
Kitu kingine muhimu ni kuhusu matembezi na kadi yako ya benki. Siku hizi kuna maendeleo ya teknolojia kiasi kwamba fedha inaweza kupatikana katika vibanda vya kutolea fedha (ATM) au hata kupitia mitandao ya simu za mikononi.
Jifunze kuacha kadi ya ATM nyumbani ili kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kujitokeza na kukufanya ufikirie kwenda kutoa salio na ikiwa haina budi, ni jambo la busara kuacha kujiunga na huduma za fedha katika mitandao ya simu kwa ajili ya kujiweka sawa
