MBINU ZA KUWA MTU MAARUFU KATIKA JAMII

No Comments
Tajiri William Henry "Bill" Gates III.
Mpenzi msomaji wangu, wiki ya nne ya darasa zuri inamalizika leo, kwa kuangali baadhi ya vipengele muhimu vinavyoweza kusaidia mtu kuwa na umaarufu kwenye jamii. Soma kwa umakini mkubwa kuanzia pale tulipoishia wiki iliyopita.
Wachagulie watu kitu kitakachokunufaisha
Ulaghai mzuri zaidi ni ule unaoonekana kuwapa watu wengine chaguo la jambo la kufanya.  Maadui zako watahisi wako huru kumbe ni vikaragosi wako. 
Wape watu chaguo ambalo litakunufaisha.  Walazimishe wachague kitu ambacho kitakupa faida.  Waweke katika hali ambayo watashindwa kujitoa bali waendelee kukunufaisha.
Jione mfalme na watu wakuone hivyo
Jinsi unavyojiona ndivyo watu watakavyokuchukulia pia.  Ukijipa mwonekano wa ovyo watu watakuona mtu wa ovyo na kutokuheshimu.
Mfalme hujiheshimu na huwafanya wengine kuwa na hisia hizo pia.    Kwa kufanya mambo kama mfalme na kujiamini, ni dhahiri unajipalilia njia ya kuvishwa taji la mafanikio.
Jua kuutumia muda wako
Kamwe usitake kuonekana una haraka, kuharakisha mambo kunakufanya ushindwe kujidhibiti na kuudhibiti muda.  Siku zote onekane huna haraka, kama vile unajua kila kitu kitakamilika.  Ufahamu wakati muafaka wa kufanya jambo, fahamu nguvu ya muda na njia ambazo zitakuletea mafanikio.    Jifunze kusubiri wakati muda haujafika na kuutumia ipasavyo wakati unapowadia.
Chukia vitu ambavyo hutavipata, vidharau
Kukubali tatizo dogo likukere ni kulikuza na kulifanya liaminike.  Unavyozidi kumfikiria adui yako ndivyo unavyomfanya awe na nguvu zaidi.  Tatizo dogo huwa kubwa zaidi na lenye kuonekana zaidi unapojaribu kulitatua. Wakati mwingine ni kuyaacha mambo kama yalivyo. 
Kama kuna kitu unakitaka na huwezi kukipata, kidharau.  Unavyokipuuza ndivyo unavyozidi kujipunguzia matatizo.
Fikiri unavyotaka lakini ishi kama wengine
Ukionekana kwenda kinyume na nyakati, ukaacha tabia  na mazoea yako ya siku zote, watu watafikiri unataka kuvutia nadhari yao na kwamba unawadharau. 
Watatafuta njia ya kukuadhibu kwa kuwafanya waonekane si lolote kwako.    Ni vyema kuendelea na tabia yako ya siku zote.  Endeleza tabia yako halisi na marafiki zako.
Mchokoze adui ili umfahamu  undani wake
Chuki na munkari huzaa hasara.  Ni lazima uwe mtulivu na mwenye busara.  Lakini ukiweza kumuudhi adui yako na ukabaki umetulia, jambo hili linaweza kukuletea faida.  Mchokoze adui yako kwa kumuudhi ili uweze kumtambua alivyo.
Kataa vitu vya bure
Vitu vinavyotolewa bure huwa ni vya hatari, kwani hujumuisha njama fulani au malengo yaliyojificha.  Kilicho na thamani basi kigharamie.
Kwa kununua kitu utakuwa umejipa furaha, ukakwepa kujiona una deni au kulaghaiwa.  Ni vyema kitu ukakinunua.  Tumia fedha zako kikamilifu kwani ukarimu ni sumaku inayovuta nguvu.
Epuka kutumia mafanikio ya waliokutangulia
Kinachotokea kwanza siku zote huonekana chema zaidi na chenye asili zaidi kuliko kinachofuata.  Ukimrithi mtu maarufu au mzazi maarufu, utalazimika kupata mafanikio mara mbili zaidi kuliko yake.
Usipotelee katika vivuli vyao bila ya wewe kufanya lolote. 
Jenga jina lako na utambulisho wako kwa kubadili mwelekeo.  Yafute majina ya waliokutangulia kwa kujenga nguvu yako mwenyewe.Watenge wachochezi katika jamii
Matatizo mara kwa mara huanzia kwa mtu mmoja.  Ukiwapa nafasi watu hawa kufanya wanavyotaka, watu wengine watawafuata.
Usisubiri matatizo yakaongezeka, usijaribu kujadiliana nao, kwani haiwezekani.   Zivunje nguvu zao kwa kuwatenga au kuwafukuza adui zako mahali ulipo, usikubali wawaambukize wengine ubaya wao.
Wavunje nguvu, waudhi maadui kwa kuwalaghai
Kioo huonyesha taswira ya kweli, lakini bado kinaweza kutumika kama chombo cha ulaghai.  Ukifanya mambo ambayo maadui zako wanayafanya, watakuwa hawawezi kujua mikakati yako. 
Watafikiri unashirikiana nao katika yale wayafanyayo.  Ni watu wachache wanaoweza kukwepa nguvu za kioo cha taswira kufanya kama vile mshika kioo anavyofanya kwa kujiona.
Hubiri nia ya mabadiliko, usibadili mambo mengi mara moja
Kila mtu hufahamu haja ya mabadiliko.  Kutokana na tabia ya binadamu, mabadiliko mengi huleta kero na upinzani.  
Ukiwa katika wadhifa mpya, mgeni au ukitaka kujenga msingi wa madaraka, heshimu taratibu za zamani ambazo zipo.  Kama mabadiliko ni ya lazima, basi yafanye yaonekane kama ni  maboresho tu ya mambo ya zamani, usibadilishe mambo harakaharaka.
Epuka kuonekana unafahamu mno
Kuonekana wewe ni bora zaidi ya wengine ni jambo la hatari, lakini jambo la hatari zaidi ni kuonekana huna makosa au unyonge wowote.  Wivu hujenga maadui wa kimya.  Ni vyema kila mara kuonyesha makosa yako na kukiri makosa ambayo hayana madhara ili kuepusha wivu na uonekane na wewe pia ni binadamu kama wengine.
Ni miungu tu na wafu ndiyo wanaweza kuonekana hawana dosari.
Usivuke malengo yako; upatapo ushindi jifunze ni lini unapaswa kusimama.
Wakati wa ushindi ni wakati wa hatari zaidi. 
Ushindi unapopatikana, maringo na kujiamini zaidi vinaweza kukusukuma ukapitiliza katika lengo ulilojiwekea.  Kwenda mbali mno kutakujengea maadui wengi zaidi ambao hutaweza kuwashinda.  Usikubali kulewa ushindi.  Heshimu mikakati na mipango yako.  Jiwekee lengo, unapolifikia simama hapohapo kwanza kabla ya kusonga mbele tena.
back to top