KUNA KITU ZAIDI YA NENO NAKUPENDA-2

No Comments

NI wakati mwingine tena tunakutana katika safu yetu nzuri ya kuelimishana juu ya uhusiano na mapenzi. Ni matumaini yangu kuwa umekuwa ukijifunza vitu vipya kila siku.

Leo tena unakwenda kujifunza kitu kipya.
Somo letu linatokea wiki iliyopita tukiongozwa na kichwa; kuna kitu zaidi ya neno nakupenda? Wengi huchanganya maana lakini ukweli ni kwamba, nyuma ya neno nakupenda kuna maana nzito na kubwa sana kwa wapenzi.
Tayari tulishaanza na vipengele vilivyotangulia, hebu sasa tuendelee pale tulipoishia wiki iliyopita...
KWANZA JITAMBUE
Lazima ujitambue, ujue nafasi yako kwa mwenzako kisha uhakikishe unasimama sawasawa. Usipojitambua hutaona thamani ya mapenzi, hutaona umuhimu wako kwenye ndoa. Muunganiko wenu hautakuwa wa maana kama hutatambua thamani yako.
Lazima mwanamke asimame katika nafasi yake, na mwanaume naye asimamie nafasi yake. Kuna baadhi ya watu wakishaingia kwenye ndoa wanaona kila kitu kimeshaisha.
Hawaoni umuhimu wa kufikiria kuwa bora zaidi kwenye ndoa.
Ndugu zangu, nyumba inajengwa tena inajengwa kwa umakini wa hali ya juu sana. Huwezi kumuona mwenzako mpya kama wewe mwenyewe hujaonyesha upya katika mambo yako. Mvute mwenzi wako ili akuone kweli unahitaji kuwa mpya, hapo utatengeneza nafasi kwake kubadilika kwenye nyendo zake.
TAFUTA FURAHA YA MWENZAKO
Kati ya mambo yanayoharibu ndoa ni pamoja na kugombana mara kwa mara. Kuna wengine huwa hawawezi kuzungumza sana, kama umemkosea, ataishia kukuambia mara mbili au tatu, baada ya hapo anaamini umeelewa.
Ikitokea ukajua umekosea na mwenzi wako amekujulisha au ukamuona hana furaha, ni jukumu lako kuhakikisha furaha yake inarejea tena. Mpeleleze, jichunguze, ni wapi umekosea. Haraka sana unachukua hatua ya kurekebisha makosa yako. Usiruhusu mwenzako anune muda wote kwa sababu yako. Tafuta amani ya mwenzako.
JUTIA MAKOSA
Hakuna kitu kinachoumiza kama mmoja anapokosea na akajua mwenzake anajua kuwa amekosea halafu aache kulipa uzito tatizo hilo. Binadamu tumeumbwa na maumivu moyoni. Ikiwa mwenzako amekukosea na akabaki kimya, maumivu yake huwa mara mbili.Mwingine anaweza kufikia hatua ya kuzungumza na mwenzake kuhusu tatizo husika akitarajia atamsikiliza na pengine kukaa chini na kujadiliana pamoja lakini inakuwa kinyume chake.
MSISIMKO WA MAHABA
Rafiki zangu, usishangazwe na tatizo la msisimko wa mahaba. Ni kutokana na makosa ambayo unayafanya kwenye uhusiano wako. Wakati mwingine, unaweza kuwa chanzo au mwenzi wako akasababisha hilo kutokea.
Hali hiyo ikitokea, kamwe usiwaze kuhusu kuachana. Achana na fikra za talaka, si kwamba umemchukia mwenzi wako, si kweli kuwa mapenzi ndiyo yanakuwa yameisha. Mapenzi yapo moyoni, hivyo kamwe usiwaze kuachana kunapotokea matatizo ya namna hiyo kwenye uhusiano.
NINI CHA KUFANYA?
Jambo la kwanza kabisa kuliingiza ubongoni mwako ni ufahamu kuwa tayari kuna tatizo katika ndoa yenu. Tatizo ambalo linahitaji utatuzi wa haraka sana.Katika utatuzi wenyewe, kunawahitaji wote lakini ikitegemea zaidi upande wako kwa sababu tayari umeshagundua kuwa kuna tatizo.
Chunguza tatizo
Lazima ujichunguze, angalia nyumba yako kwa makini. Mchunguze mwenzi wako, kisha ujue ni wapi kwenye makosa. Kujua chanzo ni mwanzo wa kuelekea kwenye kutafuta ufumbuzi wenyewe. Huwezi kupata majibu kabla hujajua unachoulizwa kwenye mtihani.
Hivi ndivyo ilivyo hata katika maisha ya uhusiano ya kila siku. Ukitaka kuwa mshindi, unatakiwa kuingia kwenye mchezo unaoujua! Chunguza kwanza!
back to top