MAPENZI NI AFYA, NENDA NAYO VIZURI UISHI, UKIKOSEA NI KIFO CHA HARAKA

No Comments
Changanua mambo inavyotakiwa, kadiri unavyoyafanya maisha yako kuwa na majanga, ndivyo na umri wako unavyoufupisha. Hii ikupe changamoto ya kuchagua jema kati ya mambo mawili. Kuongeza siku za kuishi au kuzipunguza na kukielekea kifo cha haraka.
Mantiki hapa ni namna ya kuyatumia mapenzi ili kupata umri kulingana na namna utakavyokadiriwa na Mwenyezi Mungu. Vilevile, ni jinsi unavyokwenda kinyume nayo, matokeo yake yakakufanya umri wako upungue. Hapa naomba nisisitize kuwa mada hii ni muhimu sana!
Hapa hakuna maana ya matumizi ya ARV ambayo humuongezea siku za kuishi mwathirika wa VVU, muongozo ninaoutoa hapa ni namna bora ya kuyatumia mapenzi ili uweze kuishi kwa furaha. Hii ni kwa sababu furaha huleta amani ya moyo. Mapenzi yakikuendea mrama, utulivu wa moyo utautoa wapi?
Moyo unapokuwa na amani, inakuweka huru kutoka kwenye msongo wa mawazo. Inakulinda na shinikizo la damu kwa sababu ya utulivu unaokuwa nao, unawezesha moyo kufanya kazi yake ya kusambaza damu kwenye kona mbalimbali za mwili kama inavyotakiwa.
Inapotokea moyo unashindwa kufanya kazi sawasawa, hutengeneza sumu hatari kwenye mishipa ya damu, huathiri na kuharibu kabisa mzunguko wa damu kwenye ubongo, hivyo kusababisha oksijeni ikose mtiririko mzuri na baada ya hapo ni madhara makubwa ya kiafya kama siyo kifo.
Kumbe sasa mapenzi ni afya, utayaona matunda yake endapo tu utakwenda nayo vizuri. Unapaswa kuhakikisha moyo wako unakuwa huru kila siku (au kwa kadiri ya muda mrefu) ili kuondoa msongo kwa ajili ya usalama wako. Unachotakiwa kufanya ni kujitahidi kubadili misongo ya mawazo kuwa furaha. Inawezekana!
Kanuni kuu ya kuhakikisha unafanikiwa kwenye lengo lako ni kusimama katika muongozo huu: Penda unapostahili, wekeza penzi lako kwa mtu anayestahili. Macho na tamaa visikupoteze njia, mengi uyaonayo ni fahari ya macho tu. Kila siku ni vema ujifunze kutofautisha kionwacho machoni na kifaacho moyoni na maishani.
Ndugu wengi waliodanganywa na tamaa ya macho, wakaingia kichwakichwa, wameshatangulia mbele ya haki, wengine wanaendelea kuteseka na dunia. Hakikisha unayempenda, anakuwa ni yule anayeweza kurejesha upendo unaompa. Mapenzi yaliyo katika mtiririko sawia ni yale unayopokea barabara kama ambavyo wewe unatoa (give and take).

Hakikisha unayewekeza mapenzi kwake, naye yupo tayari kwa ajili yako. Penzi la upande mmoja huzaa matokeo mabaya. Hugeuka mateso makubwa kwako, huumiza moyo kabla ya kusababisha madhara ya kiafya kama nilivyotangulia kueleza hapo awali. Muombe sana usipoteze dira kwa sababu ya mapenzi.
Unaweza kuteseka na kuishi na maumivu yasiyomithilika kwa sababu ya matendo ya yule unayempenda. Dunia ilivyo mbaya ni kwamba kadiri unavyomuonesha mwenzio mapenzi ndivyo na yeye anavyozidisha maringo ambayo hukusababishia adhabu kali sana moyoni. Mtambue mapema yule mwenye mapenzi ya kujisikia!
Aliye na mapenzi ya kujisikia elewa kuwa hajitambui. Mtu asiyejitambua atakutesa sana katika maisha yako kama utaendelea kumng’ang’ania.
back to top