MAJONZI MAZITO IKULU

No Comments
MAJONZI mazito yameikumba Ofisi ya Rais, ikulu jijini Dar es Salaam kufuatia kutokea kwa vifo viwili vya watumishi wa ofisi hiyo wiki iliyopita.

 
Picha ya marehemu Rashidi John Chilwangwa (45).
Wa kwanza ni Afisa Usalama wa Taifa Mwandamizi, Silvanus Adriano Mzeru (56) aliyeuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Aprili 29, mwaka huu  maeneo ya Uwanja  wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar.
 
Picha ya Marehemu ambaye alikuwa Afisa Usalama wa Taifa Mwandamizi, Silvanus Adriano Mzeru (56).
Gazeti hili lilifuatilia habari hiyo na kunasa madai kwamba  wauaji  hao walikuwa na  pikipiki aina ya Boxer. Ilielezwa kuwa wadunguaji hao walimfuatilia afisa huyo tangu maeneo  ya Tazara jijini Dar.
Ilidaiwa kuwa, kufika eneo hilo la uwanja wa ndege, taa za kuongozea  magari  zilionesha ishara ya magari yanayotokea mjini  yanatakiwa kusimama lakini baada ya dakika kama mbili taa hizo  ziliruhusu  magari kuondoka.
 
MKe wa Silvanus Mzeru kushoto pichani.
Ndipo ghafla  watu hao waliokuwa wamejibanza sehemu walimmiminia risasi marehemu  upande  wa mbele wa kioo na kumfanya  apoteze  uelekeo  na gari  lake  aina  ya Toyota Land Cruiser lenye  namba za usajili T 844 CUG kwenda  kuligonga kwa nyuma gari  lingine lenye  namba T 786 BLS.
 
Mama Salma Kikwete (mbele) na akina mama wengine wakiwa katika hali ya majonzi.
“Cha ajabu sasa, baada ya kufanya kitendo kile, wale watu  kwanza walipiga risasi hewani ili raia wasisogelee  eneo  la  tukio. Halafu ndani ya gari la marehemu  walikuta pesa ambazo kiwango chake hakijafahamika na ‘brifkesi’ inayodaiwa ilikuwa na nyaraka mbalimbali,” kilisema chanzo.
Ukiachana na mauaji ya afisa usalama huyo, mfanyakazi mwingine wa ikulu, Rashid John Chilwangwa (45) naye alikutwa na mauti baada ya kuanguka ghafla.
 
Mwili wa Silvanus Mzeru wakati akisindikizwa kwa safari yake ya mwisho.
Chilwangwa alifariki dunia  ghafla saa 4:20, Mei Mosi, 2014 ndani ya Uwanja wa Uhuru  wakati sherehe za siku ya wafanyakazi duniani zikiendelea.
 
Ibada ya kumuaga marehemu Silvanus Mzeru.
Waandishi wa habari walikuwepo katika eneo la tukio na kushuhudia wafanyakazi wa ikulu na wananchi wengine wakitokwa machozi mara baada ya kupokea taarifa  za kifo hicho kutoka kwa wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu waliokuwa wakijaribu kuokoa uhai wake.
Baadaye ilidaiwa kuwa, marehemu alikuwa akisumbuliwa na kisukari na siku ya tukio, presha yake ilipanda.
 
Mwili wa Chilwangwa uliagwa Ijumaa iliyopita nyumbani kwake, Mabibo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo mke wa rais, mama Salma Kikwete (    pichani).
Marehemu Chilwangwa alizikwa Ijumaa hiyohiyo, Kisarawe, Pwani huku marehemu Mzeru akizikwa Mei 3, mwaka huu kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mungu azilaze pema peponi, roho za marehemu hao. Amina.
back to top