Mbwembwe zatawala urejeshaji fomu Chalinze

No Comments


Bagamoyo. Mbwembwe na tambo za kisiasa pamoja na shamrashamra mbalimbali zimetokea jana katika Ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Chalinze baada ya wagombea ubunge jimbo hilo kurejesha fomu zao za uteuzi wa ubunge.
Mgombea wa kwanza kurejesha fomu ni mteule wa Chama cha Wananchi CUF, Fabian Skauki ambaye alifika saa 5.37 asubuhi na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Samwel Sarianga alizithibitisha kuwa hazina dosari yoyote.
Saa 7.46 mgombea wa CCM, Ridhiwan Kikwete naye aliwasili kwenye ofisi hiyo kurejesha fomu zake, huku akisindikizwa na umati mkubwa wa wanachama akiwamo hasimu wake wa kura za maoni, Iman Madega.
Wagombea wengine waliorudisha fomu zao ni pamoja na Chadema waliowasili ofisini hapo huku mgombea wao Mathayo Torongey akisindikizwa kwa nyimbo na ngoma za asili na makada wa chama hicho. Wengine ni wa Chama cha AFP, Ramadhan Mgaya aliyerudisha saa 9:45, huku mgombea wa NRA, Muniru Hussein akirudisha saa 9:55.
back to top