KWA NINI WANAUME WENGI SIKU HIZI HAWAPENDI KUOA...?

No Comments


Kumekuwa na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa jamii
 kwamba imekuaje vijana wa kiume wamekuwa ni waongo sana
 hasa linapokuja swala la kuoa? Kwa kadiri siku zinavyozidi kwenda
 ndivyo ambavyo idadi ya wanaume wanaoogopa kuoa inazidi 
kuongezeka. Utakuta wapenzi wanaambiana kwamba wanapendana
 na kuahidiana kuwa wataoana, lakini kitakachotokea baada ya hapo
 ni mwanaume kuanza kupiga chenga kwa visingizio lukuki.

Kwa nini hali hiyo hutokea?

Ukweli ni kwamba hakuna jibu la moja kwa moja juu ya tatizo 
hilo, lakini yapo mambo ambayo yanaweza kutupa angalau 
tafakuri. Nitajaribu kudadavua baadhi ya sababu zinazowafanya
 wanaume siku hizi kukwepa kuingia katika taasisi ya ndoa:



1 Ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano: Hapa
nawazungumzia wale watoto wa kiume waliolelewa malezi ya 
upande mmoja yaani walilelewa na mama peke yao. Sina maana
 ya kudharau au kutweza malezi ya mama, la hasha, lakini ni
 vyema mkafahamu kwamba kuwa na baba asiye na malezi 
mazuri si sawa na kutokuwa na baba. Na ndio maana nikasema 
ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano. Achilia mbali aina
 ya malezi atakayoyapata kwa familia yawe mazuri au mabaya lakini
 lazima kutakuwa na tabia za kiume zitakazoakisi malezi ya mtoto
 wa kiume katika familia husika. Watoto waliolelewa na mama 
peke yao kuna kitu huwa wanakosa, kwani wanakuwa hawana 
mtu wa kumchukulia kama mfano kwa upande wa jinsia ya 
kiume na hapo ndipo hujikuta wakijifunza wenyewe namna
 ya kuongea na kutenda kama wanaume kwa sababu katika
 makuzi yao hawakupata fursa ya kuwa karibu na baba zao.
 Kwa kuwa siku hizi kuna kundi kubwa la kina mama ambao 
wamejikuta 
wakiachiwa mzigo wa malezi ya watoto, baada ya aidha 
kuachwa na waume zao au kuzalishwa na 
kutelekezwa (Single mothers), na hapo ndipo 
tunaposhuhudia mtoto wa kiume anapokua kwa 
umri na kimo huku akiwa hana mtu wa kumuangalia 
kama mfano wa mume anavyotakiwa kuwa katika
 familia zaidi ya kujifunza mambo hayo kupitia katika TV,
 senema au miziki. Wanaume waliopitia malezi ya aina hii
 huchelewa sana kuoa kwani huyaangalia maisha ya ndoa
 kwa namna ya kujaribu na ndipo hapo wengi huishia kuishi
 kinyumba na wanawake kwa ajili ya kutaka kujifunza
 namna ya maisha ya ndoa yanavyotakiwa kuwa na ndio
 sababu huchukua muda mrefu kufanya maamuzi.
 Na mara nyingi huishia kubadilisha wanawake 
kutokana na kutokuwa na uhakika wa kile wanachokitafuta.



2 Mgogoro wa kiuchumi: Kuna kundi kubwa la
 vijana siku hizi hawana ajira au hawana uhakika na
 kipato. Ukweli ni kwamba hakuna mwanaume 
atakayependa kujiingiza kwenye ndoa wakati
 hana kazi au hana uhakika na kipato chake. 
Na hiyo ni kutokana na wanawake wengi siku
 hizi kuonekana kujali zaidi wanaume wenye
 uhakika na kipato. Hii misemo ya wanawake 
ya kebehi dhidi ya wanaume wasio na ajira au kipato,
 kama vile “mwanaume suruale” ina mchango mkubwa
 sana katika kuwafanya wanaume kukwepa kuoa iwapo
 hawana ajira au hawana uhakika na kipato chao.





3 Wanawake wengi kuwa na kiwango cha elimu ya juu:
 Siku hizi wanawake wengi wameibuka katika kutafuta elimu ya
 juu kwa juhudi kubwa. Idadi ya wanawake 
wanaojiunga na vyuo vikuu ni wengi tofauti
 na ilivyokuwa zamani. Na hiyo ni kutokana 
na wazazi wengi kubadili mtazamo wao juu
 ya mtoto wa kike. Zamani mtoto wa kike 
alichukuliwa kama kitega uchumi.
 Kwa maeneo ya vijijini na katika familia masikini,
 watoto wa kike walikuwa wanatazamwa kama,
 ‘biashara ya kesho’ ambapo watauzwa kwa njia ya mahari.
 Kwa hiyo thamani yao ilikuwa ni kuolewa,
 ni ile ya kibidhaa na sio kibinadamu. 
Lakini tofauti na zamani siku hizi hata
 kule vijijini kumekuwa na mwamko
 mkubwa sana wa kumsomesha mtoto
 wa kike hadi elimu ya juu.
 Kutokana na mwamko huo wanawake wengi 
wamejikuta wakiona elimu kama kimbilio pekee 
la kuepukana na mfumo dume. Mwanamke gani
 atakubali kunyanyaswa na mwanaume akiwa na
 elimu yake na labda pia akiwa na kazi yake yenye
 mshahara na marupurupu ya kutosha, naamini
 watakuwa ni wachache sana ambao hawajiamini
 au waliathiriwa na malezi. Kwa upande wa wanaume
 nao, wamejikuta wakiwaogopa wanawake hawa wenye
 elimu ya juu kwa hofu ya kuzidiwa kipato na labda 
kukosa sauti kama mwanaume na hiyo inatokana na ego tu.



4 Wanaume huwaona wanawake kama tishio
 wanapokuwa na mafanikio makubwa kifedha: Inaweza
 kutokea mwanaume anaweza kuwa na uhusiano na 
mwanamke ambaye labda tu nisema ni mbangaizaji. 
Wakati huo anaweza kuahidi kufunga ndoa na 
mwanamke huyo, lakini iwapo itatokea mwanamke
 huyo akapata mafanikio kibiashara na kuinuka kifedha. 
Kama mwanamke asipokuwa makini anaweza kusababisha
 mwanaume huyo akaingia mitini. Sababu kubwa hapo
 inaweza kuwa ni hofu ya kuogopa kuongozwa na mwanamke.
 Kumbuka kwamba mfumo dume bado umetawala 
vichwani mwa wanaume wengi kutokana na malezi.
 Mwanaume asiyejiamini ni vigumu sana kwake kuoa
 mwanamke aliyemzidi kipato. Kwa sababu akifanyiwa
 jambo dogo tu, inakuwa kama ametoneshwa.
 Atahisi kutaka kutawaliwa na mwanamke huyo.
 Jambo ambalo wanawake wanatakiwa
 kulifahamu ni kwamba kila mwanaume
 anataka kutambuliwa na kuheshimiwa
 kama shujaa kabla ya kumfuata msichana. 
Iwapo utakuwa umesimama iwe ni kifedha au kielimu
 pale unapotafuta kupata mwenza, inabidi ujishushe
 sana la sivyo utadoda.





5 Wanaume wengi siku hizi wana hofu ya majukumu,
 hasa ya kulea watoto: Kutokana na malezi yao au
 kile wanachokijua kuhusu watoto, baadhi ya 
vijana huamini kwamba, kulea watoto ni jambo gumu sana.
 Lakini wengine wanaamini kwamba, hata mke anapaswa 
kulelewa kama ilivyo kwa mtoto. Hivyo wanaamua kutafuta 
kwanza uwezo ambao haupatikani kiurahisi. Kuna wengine,
ambao wamefundishwa au kuelekezwa na mila na desturi
 zao kwamba, kabla hawajaoa, ni lazima wawe na nyumba
 kwanza, tena kwao. Kwa hiyo, hawa hadi waje wapate uwezo 
wa fedha wanakuwa wameshachelewa.



6 Kuna baadhi ya wanaume, maisha
 bila ya ndoa wanayaona kuwa ndiyo bora
 kuliko yale ya ndoa: Kuna baadhi ya 
wanawake hujirahisisha sana kwa wanaume. 
Siku hizi ni jambo la kawaida sana kukuta
 mwanaume anaishi na mwanamke bila ndoa,
 wenyewe wanaita Trial Marriage. 
Na hapo ndipo unapokuta wanaume 
hawaoni tena umuhimu wa kuoa.
 Sasa kama mwanamke anaweza 
tu kuishi na mwanaume bila ya 
ndoa na mwanaume huyo akapata
 huduma zote kutoka kwa mwanamke
 huyo, unadhani ni kitu gani kitamvuta
 kufunga ndoa. Jambo lingine ni ile dhana
 kwamba maana ya ndoa ni tendo la ndoa. 
Siku hizi wanaume wengi wamejikuta wakiwa hawahitaji
 tena kuoa kwa sababu tendo hilo linapatikana kiurahisi
 tofauti na zamani. Siku hizi ina
wezekana kabisa kumtongoza binti leo na
 kupata tendo siku hiyo hiyo….. 
Na hapa siwazungumzii makahaba. 
Nawazungumzia mabinti zetu ambao 
wengine ukiwaona ni watu wa kuheshimiwa
 ukiwaangalia kwa nje lakini kwa ndani hawana
 lolote, vijana wa siku hizi wenyewe huwaita maharage ya Mbeya.



Kuna sababu nyingi zinazotajwa kusababisha wanaume 
siku hizi kujivuta sana katika kufanya maamuzi ya
 kutafuta mwenza. Lakini hizo chache nilizozitaja
 zina mchango mkubwa.

back to top