Abdulaziz Chende 'Dogo Janja' kutoka Ngarenaro.
ABDULAZIZ Chende ndilo jina lake halisi alilokuja nalo jijini Dar es Salaam akitokea Ngarenaro, kule mjini Arusha, lakini wajanja wa mjini wakambatiza kama Dogo Janja, ambalo kwa kweli limemkaa vyema.
Ni bwana mdogo kweli, siyo tu kwa umri, bali hata sanaa aliyoichagua. Ni kijana ambaye kwa jinsi watoto wa Dot.com walivyo, alistahili kuwa kidato cha kwanza, pili au hata cha tatu. Ulimwengu wa Bongo Fleva, ulimtambua baada ya kutambulishwa na Kundi la Tip Top Connection, kupitia kwa kinara wake, Madee.
Dogo janja akiwa mzigoni.
Dogo anaweza kurap. Lafudhi yake ya watoto wa Kiarusha inamuongezea ‘credit’ katika muziki wake, kwa sababu nayo ni kitambulisho kingine cha uwepo wake. Wakati akitambulishwa, Madee aliwaahidi mashabiki kuwa atamlea Dogo katika njia inayofaa, ikiwa ni pamoja na kumkuza kisanii na kielimu.
Simulizi zilisema alipelekwa Makongo Sekondari jijini Dar es Salaam. Ghafla ukaibuka mzozo mkubwa baina ya Dogo na Madee, uliosababisha Chalii kurudi zake Arusha. Sina sababu ya kurudia maneno yaliyoibuliwa na pande zote mbili wakati ule kila mmoja akijisafisha mbele ya macho ya watu.
Lakini kifupi Dogo Janja alilia kufanywa mgodi, akitumika kumtengenezea hela Madee, kwamba alipiga shoo nyingi, lakini kipato akawa hakioni, kinaishia kwa mkubwa. Na Madee naye alifunguka, akimlaumu Dogo kwa kuzuzuka na jiji, kuacha shule na tabia nyingine mbaya.
Kwa sababu zilizo wazi, watu wengi walimuunga mkono Dogo Janja, wakamsifu kwa kujitambua. Lakini bahati mbaya, baada ya kutoka Tip Top, akadondokea Mtanashati Entertainments ambako baadaye taarifa zilisema alifukuzwa kwa makosa yanayofanana na yale yaliyowahi kutolewa na Madee.
Habari ambazo bado hazijathibitishwa, zinasema kijana wetu amenyoosha mikono, anataka kurejea tena Tip Top Connection, kule kule ambako ‘Rais wa Manzese’ ndiye mfalme.
Kama nilivyosema pale awali, Dogo Janja bado ni kijana mdogo kwa umri. Sanaa aliyochagua inahitaji mtu aliyetulia kichwani ili aweze kufanikiwa. Kitu ambacho kingeweza kumsaidia kupata mwongozo bora katika maisha yake, ni elimu pekee.
Ni jambo linalosikitisha kusikia kwamba anakimbia shule. Wakati flani nilisikia alifeli sana katika mtihani wake, sababu kubwa ikiwa ni kushindwa kuhudhuria vipindi darasani. Kama angetambua kuwa ujinga alionao, ambao yeye anauona ujanja, ndiyo unaomfanya asiende shule, hakika angetazama maili nyingi zaidi mbele na kujirudi.
Muziki wa Bongo umejaa dhuluma kila upande na watu hawa wabaya wamejenga mtandao wa kulinda masilahi yao. Mtandao huu unawahusisha watayarishaji wa muziki (producers), viongozi wa makundi, watangazaji wa redio, maofisa masoko wa kampuni kubwa na hata wasambazaji wa kazi za wasanii.
Msanii anatakiwa kuwa na kichwa kilichotulia kuweza kuushinda mtandao huu. Ndiyo maana wasanii wakubwa kama AY na Mwana FA, licha ya ustaa wao, walitumia sehemu ya mapato yao kurudi shule kujiweka sawa.
Msanii akikorofishana na mmoja kati ya wanamtandao, anaathirika sana. Kwa sababu harekodiwi nyimbo nzuri, kazi yake haichezwi redioni na wala hapewi nafasi ya kufanya shoo.
Kama angekuwa na elimu ya kujitambua, angegundua kwamba wasanii wote, akiwemo Madee mwenyewe wanaibiwa. Unafikiri hawa wanaoongoza makundi wana mapenzi gani na wasanii wawasaidie kutoka, wao wakale wapi?
Kama angekuwa na elimu ya kujitambua, angegundua kwamba wasanii wote, akiwemo Madee mwenyewe wanaibiwa. Unafikiri hawa wanaoongoza makundi wana mapenzi gani na wasanii wawasaidie kutoka, wao wakale wapi?
Na kusoma siyo lazima uwe na digrii, ni kiasi cha kujitambua tu. Ni ile hali ya kujua kwamba kwa jinsi wingu lilivyo, inabidi utembee na mwavuli kwani mvua inaweza kunyesha wakati wowote.
Dogo Janja bado hajachelewa, anao muda mzuri tu wa kuelimika, tena kwa fedha zake mwenyewe. Ningekuwa mimi katika nafasi yake, nadhani ningefanya maajabu, maana muziki ungenipatia elimu ambayo ingeboresha maisha yangu kwa kiwango cha juu kabisa, umri na uwezo wake ni mtaji ambao wengi wanautamani.
Kama amechagua kutembea katika njia hiyo, ambayo kwa bahati mbaya kaka na dada zake nao wanapita, tusitarajie kuwepo kwa mabadiliko, siyo tu ya muziki, bali hata wasanii wenyewe.
Kila siku tutawashuhudia wakiwasujudia watu ambao walipaswa kuwanyenyekea.
Kila siku tutawashuhudia wakiwasujudia watu ambao walipaswa kuwanyenyekea.