ATHARI ZA KUHARAKISHA FARAGHA-4

No Comments
KUJIFUNZA hakuna ukomo. Ni vyema kujiwekea utaratibu wa kujifunza kila siku. Maana yake katika kujifunza huongeza maarifa.
Ulichokuwa ukikifahamu jana, huenda leo ukajifunza kitu kingine tofauti. Hapa kwenye Love & Life tunajifunza mambo muhimu kuhusu maisha yetu.
Vijana wa sasa wanaamini faragha huongeza na kuimarisha penzi. Jambo hili halina ukweli, kuna mambo mengi muhimu zaidi ya faragha ambayo yakifanywa huzidisha furaha ya uhusiano.
Zipo athari (hasa kwa wanawake) ambazo wanaweza kuzipata kama wakiharakisha faragha. Leo tupo katika hatua ya mwisho. Wiki iliyopita niliishia pale nilipozungumzia kuhusu mimba bila kutarajia.
Kwa bahati mbaya sana, wanawake wengi wakiwa faragha huwa hawafikirii kabisa suala la kupatikana kwa mimba.
Mbaya zaidi huwa hawajiandai kwa kuwa na kinga ya kuzuia upatikanaji wa mimba bila mpangilio.
Kwa kawaida, msichana anayejitambua hufahamu mzunguko wake wa hedhi ulivyo na siku za hatari kwake kupata mimba, hivyo ana uwezo mkubwa wa kutambua siku ambazo si sahihi kukutana na mwanaume.
Mimba ni mtoto mtarajiwa. Huwezi kubeba mimba kwa bahati mbaya, maana mtoto huandaliwa (na wazazi wake wote wawili). Kukurupukia faragha ni chanzo cha kuingia kwenye tatizo hilo.
Ni tofauti na yule ambaye tayari ana ndoa yake. Huyu atakuwa anafanya tendo la ndoa. Kupata mimba ndani ya ndoa ni sehemu ya ukamilifu na furaha ya ndoa hiyo.
Hapo sasa unaweza kuona tofauti. Aliye kwenye ndoa anafurahia, aliye nje ya ndoa anawaza kuitoa. Huko kwenye kutoa nako kuna matatizo kibao.
(VI) Magonjwa
Ukiacha hatari ya kupata magonjwa ya zinaa pia kuna suala la ujauzito.Mathalani utakuta msichana amepata mimba isiyotarajiwa, anatafuta shotikati na kwenda kuitoa.
Hapo kuna matatizo mengine mengi anayoweza kuyapata kutokana na kitendo hicho.
Tendo la utoaji mimba halijahalalishwa hivyo hufanyika kienyeji. Vifaa duni (visivyo safi na salama) huweza kusababisha maambukizi katika mfuko wa uzazi.
Ukiachana na hilo, kama mimba ikitolewa vibaya (hakuna kutolewa vizuri – kuna kusafishwa kizazi kwa idhini ya daktari) mwanamke anaweza kupata ugumba.
Kwa nini uwe kwenye maisha yenye presha kiasi hicho? Ni vizuri sasa wasichana wakachukua hatua na kuwa makini kwa kila wanachokifanya kwenye uhusiano wao hasa tendo la ndoa.
back to top