Namshukuru Mungu kwa mara nyingine tena kwa kunijaalia fursa hii adhimu ya kuzungumza nanyi wapenzi wasomaji wa safu. Jamani mambo vipi? Natumaini ilikuwa bab kubwa! Au siyo!
Basi sawa, hiyo imepita ila nawakumbusha tu kwamba kuoneshana upendo isiishie Valentine’s Day tu. Tuoneshane kupendana kila siku na ikiwezekana kila siku iwe Valentine’s Day.
Baada ya kusema hayo, nirudi sasa kwenye mada yangu ya leo. Mpenzi msomaji wangu, wapo ambao wamejikuta wakiitwa wahuni kutokana na kuwa na uhusiano wa kimapenzi na makundi ya wanaume au wanawake.
Hata hivyo wachunguzi wa masuala ya mapenzi wanasema idadi kubwa ya wapenzi si kigezo sahihi cha kupima tabia ya mtu na kumhusisha na uhuni.
Watalaam hao wanataja safari ya kupata chaguo halisi la mwenza wa maisha kuwa ndiyo inayowaponza wengi kiasi cha kujikuta wameingia katika kashfa ya kuwa na uhusiano na wapenzi kibao ndani ya muda mfupi.
Wanasema msichana au mvulana anayeingia katika uwanja wa mapenzi kwa kuwa na hisia za kufanya ngono, hukosa umakini wa nani anafaa kuwa mpenzi wake kutokana na kukosa elimu ya uhusiano.
Kwa mantiki hiyo, bila upembuzi wa kina, mtu asiye na elimu ya jinsi ya kumpata mpenzi wa kweli hujikuta ameangukia kwa mtu asiyemfaa, ambapo baadaye huamua kuachana naye na kwenda kwa mwingine kujaribu bahati tena.
Zinatajwa zawadi, hitaji la kusaidiwa kimaisha, mvuto wa kimahaba na mazoea kuwa vichocheo vinavyowaingiza wengi kwenye wapenzi wasiowafaa.
Ukweli ni kwamba mtu aliyenaswa kwa ulimbukeni huo, huwa hakatwi kiu ya penzi na mtu asiye chaguo sahihi la maisha yake. Hivyo hufikia uamuzi ya kujiingiza katika uhusiano mpya mara nyingi na kujikuta wakiambulia watu walewale wasio sahihi kwao.
Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Zaituni aliwahi kuniomba ushauri, akasema amechoka kuchezewa, maana kila mwanaume anayempata anakuwa si chaguo lake. Lakini kibaya zaidi huachia ngazi au hutemwa huku akiwa tayari ameshafanya mapenzi na wanaume hao.
Nia ya swali lake ilikuwa ni kuniomba njia za kumtambua mwanaume mkweli bila kufanya naye mapenzi. Aliuliza hivyo huku akiwa na hoja kuwa wanaume wengi hawako tayari kuwa na uhusiano na msichana bila kufanya naye mapenzi na wakati huohuo huficha tabia zao chafu wakilenga kumnasa wamtakaye.
Binafsi nafahamu kuwa kuna watu wengi ambao hujiingiza katika mapenzi kwa kutekwa na hadaa za mwili na kujikuta wanacheza mchezo wa pata potea.
Labda nikuambie tu kwamba, unapompata yule ambaye moyo wako umemzimikia, jipe muda wa kutosha kati ya miezi sita na mwaka kumchunguza. Keti chini na uanze kujumlisha alama za vigezo ulivyojiwekea na jinsi mtu huyo alivyopata au kukosa.
Ukiona uliyemchagua amepata zaidi ya nusu ya alama ya vigezo ulivyoweka, tambua huyo anakufaa. Kuhusu alama chache alizokosa unaweza kusaidia kuzikamilisha polepole wakati mko ndani ya uhusiano.
Lakini pia unatakiwa kuwa makini sana pale ambapo utakayempata ataonesha kuharakisha suala la kufanya mapenzi na wewe. Kwa mfano, msichana unapokutana na mwanaume ambaye anaonesha kulazimisha penzi, huyo atakuwa amekutamani na ukimpa nafasi kwenye moyo wako, atakuja kukuliza.
Kikubwa hapa ni kujali maisha yako na kuhakisha unaepuka kuwa na historia ya kuwa na wapenzi kibao kabla ya kuingia kwenye maisha ya ndoa.
Pia epuka sana kuwa na watu zaidi ya mmoja eti kwa lengo la kuwachunguza ili mmoja wao akionekana kuwa na muelekeo, umpe nafasi.
Pia epuka sana kuwa na watu zaidi ya mmoja eti kwa lengo la kuwachunguza ili mmoja wao akionekana kuwa na muelekeo, umpe nafasi.
Hii ni hatari sana kwani kama watajuana unaweza kujikuta unachafuka kwa kuitwa malaya kumbe huenda ulikuwa na nia njema ya kuwachunguza bila kufanya nao mapenzi.
Ni vyema mbinu sahihi zitakutumika kumtambua mtu mwenye mapenzi ya dhati na wewe na katika matoleo yajayo nitaeleza kwa kirefu alama za mtu mwenye mapenzi ya kweli na yule ambaye ni msanii.
Ni vyema mbinu sahihi zitakutumika kumtambua mtu mwenye mapenzi ya dhati na wewe na katika matoleo yajayo nitaeleza kwa kirefu alama za mtu mwenye mapenzi ya kweli na yule ambaye ni msanii.
